CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Wednesday 14 June 2017

VETA na Airtel watangaza kozi 5 mpya za ufundi stadi kupitia simu za mkononi.



Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa kushirikiana na kampuni ya simu za mkononi ya Airtel kupitia application ya VSOMO  wametangaza na kuzindua kozi mpya za ufundi stadi za VETA zitakazotolewa kupitia simu za mkononi ili kuwawezesha watanzania kujiunga na kupata utaalamu na vyeti vya VETA kwa gharama nafuu.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dr. Bwire Ndazi aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo iliyofanyika katika chuo cha VETA Kipawa, alizitaja kozi hizo kuwa ni Huduma ya chakula na mbinu za kuhudumia wateja, Matengenezo ya Kompyuta, Umeme wa viwandani, Ufundi Bomba wa Majumbani, na Umeme wa magari. 


Alisema mradi wa VSOMO unaisaidia VETA kutekeleza lengo la kupanua wigo wa utoaji mafunzo na kuweza kuwafikia makundi yote katika jamii, kama inavyoainishwa katika Mpango Mkakati wake.


Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Dar es Salaam Habib Bukko alisema VSOMO imekuja wakati ambao serikali inaelekea kwenye uchumi wa viwanda na kwamba jamii inahitaji stadi stahiki ili kuweza kufanikisha azma hiyo.
Awali, Mkuu wa Chuo cha VETA Kipawa Eng. Lucius Luteganya ambaye ni Mratibu Mkuu wa mradi huo alisema wakati wa uzinduzi wa mfumo huo wa mafunzo kwa njia ya simu kupitia application ya VSOMO mwezi Juni 2016, mafunzo yalianza kutolewa katika kozi za Ufundi umeme wa manyumbani, Ufundi pikipiki, Ufundi wa simu za mkononi, Ufundi Alluminium, Utaalamu wa maswala ya urembo pamoja na Ufundi wa kuchomea vyuma.

Aliongeza kuwa, mfumo huu wa masomo kwa njia ya simu-VSOMO, sasa ni maarufu kwa vijana ambapo takwimu zinaonyesha zaidi ya vijana 30,000 tayari wamepakua application ya VSOMO, 8000 wamejiandikisha na kati yao 50 wanasoma kozi mbalimbali na wengine tayari wameshahitimu na kupata vyeti vya VETA.

“ili kupata mafunzo ya VSOMO unatakiwa kuwa na mtandao wa Airtel kisha pakua application ya VSOMO katika google play store, na kujisajili na kisha chagua kozi inayokidhi mahitaji yako,” Alisema

Eng. Luteganya aliongeza kuwa katika kuhakikisha elimu inayotolewa inakidhi viwango vya elimu vilivyowekwa na VETA, wanaofaulu masomo ya nadharia kupitia VSOMO hupaswa kuhudhuria mafunzo ya vitendo katika vituo vya VETA vilivyopo maeneo mbalimbali nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Bi Beatrice Singano Mallya alishukuru kwa VETA kuongeza kozi katika mfumo wa VSOMO.

“tunajisikia furaha kuongeza kozi nyingi zaidi katika mfumo huu wa masomo kwa njia ya mtandao wa VSOMO,kwani itatuwezesha kufikia idadi kubwa ya vijana wanaosoma kwa kupitia simu zao za mkononi. Lengo letu ni kuhakikisha tunakuwa na kozi nyingi ili kwenda sambamba na matarajio na mahitaji ya wanafunzi na watanzania kwa ujumla,” alisema









No comments:

Post a Comment