CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Wednesday 25 November 2020

Bodi ya VETA yahimiza ukamilishaji ujenzi wa vyuo vya VETA Kagera na Geita

Bodi ya Taifa ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi imehimiza ukamilishaji haraka wa ujenzi wa vyuo vya VETA Kagera na Geita ili wananchi waanze kunufaika na mafunzo katika vyuo hivyo.

Wito huo umetolewa wakati wa ziara ya Bodi hiyo katika miradi ya ujenzi wa vyuo vya VETA Kagera, VETA Chato na VETA Geita iliyofanyika tarehe 10 hadi 12 Novemba 2020 kwa lengo la kujionea uhalisia wa miradi hiyo. 

Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Ndugu Peter Maduki amesema Bodi yake inataka kuona kasi kubwa ya ujenzi wa vyuo vya VETA Kagera na VETA Geita ili hatimaye vikamilike na kuanza udahili mwaka 2021.

Alipongeza hatua zilizochukuliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika kuendeleza ujenzi wa Chuo cha VETA Geita uliokuwa umesimama kwa muda mrefu.

“Kama Bodi, tunatoa masikitiko yetu makubwa sana kwa namna ambavyo mradi umetekelezwa na kukwama kwake kwa takribani mwaka mmoja na nusu tangu ulipoanza kutekelezwa. Tunasikitika kwa sababu kubwa moja, wananchi hawawezi kupata fursa tuliyokuwa tunatarajia. Tulitarajia tungeanza kutoa mafunzo kwa wanafunzi 400 wa kozi za muda mrefu na 1000 wa kozi za muda mfupi,” amesema.

“Kama Bodi, tumetafakari jambo hili tukishirikiana na Wizara yetu ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuona namna gani tunaweza kufufua mradi huu. Hatua ya kwanza baada ya majadiliano tumeona mradi huu uendelee kwa fedha kutoka chanzo kingine ambacho Serikali imekitafuta na namna ya utekelezaji wake tumeona tuende kwa force account (kutumia nguvu na rasilimali za ndani) ambayo itatupunguzia gharama na itatuwezesha kukamilisha mradi huu kwa haraka zaidi,” ameongeza.

Amesema, hali ya uhitaji wa mafunzo kwa wananchi wa mikoa ya Kagera na Geita umedhihirishwa na kiwango cha maombi ya kujiunga na chuo cha VETA Chato ambapo zaidi ya vijana 300 wamewasilisha maombi ya kusoma kozi za muda mrefu zitakazoanza mwezi Januari, 2021.

Akitoa taarifa kwa Bodi kuhusu ujenzi wa vyuo hivyo kwa nyakati tofauti, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu amesema kuwa mradi wa ujenzi wa Chuo cha VETA Kagera umekamilika kwa asilimia 45 na unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti, 2021. Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kagera (VETA Kagera) kinajengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa gharama za fedha za kitanzania sh bilioni 19.4 katika eneo la ukubwa wa hekta 40.5 katika kijiji cha Burugo wilayani Bukoba.

Dkt. Bujulu amesema Chuo hicho pindi kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 800 wa kozi ndefu na 2000 wa kozi fupi katika fani mbalimbali ikiwemo useremala, uchomeleaji, upakaji rangi, na ufundi bomba.

Kuhusu ujenzi wa Chuo cha VETA cha Wilaya ya Chato, Dkt. Bujulu amesema miundombinu ya utoaji mafunzo kwenye chuo hicho imekamilika ikiwemo ununuzi na usimikaji wa vifaa ambapo tayari wanafunzi 60 wameanza masomo kwa kozi za muda mfupi huku wengine 300 wakiwa wamewasilisha maombi ya kusoma kozi za muda mrefu zitakazoanza mwezi Januari 2021.

Mjumbe wa Bodi ya VETA ambaye ni Rais wa Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Ndugu Paul Koyi amesema amefurahi kuona VETA ikitoa stadi zinazolenga kuandaa wahitimu watakaoweza kuanzisha shughuli zao za kuwaingizia kipato pindi wanapohitimu.

“Nimefurahishwa sana na mafunzo yanayotolewa hasa ya uchakataji samaki…Tunaahidi kuwatafutia soko la kimataifa la samaki hao wanaondaliwa kwa ustadi wa hali ya juu,” amesema.

 

No comments:

Post a Comment