CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Saturday 28 November 2020

Mbunge Festo Sanga kufadhili vijana 10 kila mwaka kusoma chuo cha VETA Makete


MBUNGE wa jimbo la Makete, Festo Sanga ameahidi kufadhili vijana 10 kila mwaka kusoma katika chuo cha ufundi cha VETA Makete na kuwataka wazazi kupeleka vijana wao kwa wingi katika chuo hicho ili waweze kujifunza fani mbalimbali.

Sanga ameyasema hayo Ijumaa tarehe 27 Novemba 2020, akiwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya sita ya Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Makete (VETA Makete).

Sanga alisikitishwa kuona mwamko mdogo wa wananchi wa Makete katika kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi licha ya kusogezewa karibu huduma hiyo ya mafunzo.

"inasikitisha kuona kati ya wanafunzi 64 wanaohitimu leo, wanafunzi wanaotokea hapa Makete hawafiki 10, zaidi ya 50 wanatoka nje ya Makete, Mara, Tukuyu, Tanga, Dar es Salaam, Iringa na kwingineko. Tafsiri yake ni kushindwa kuitumia fursa hii sisi Wanamakete. Nawaomba sana tuwalete vijana wetu hapa waje wasome,” amefafanua.

Sanga amesema kuwa Serikali imewekeza mabilioni ya fedha katika chuo hicho pekee cha VETA katika mkoa wa Njombe ili wananchi wa Wilaya ya Makete waweze kunufaika na fursa za mafunzo ya ufundi stadi, hivyo akawaomba kuitumia vyema fursa hiyo.

Sambamba na hilo, Sanga ameahidi kueneza ufahamu kwa umma juu ya mafunzo yatolewayo na VETA ikiwemo ukweli kuwa gharama zake ni nafuu na kwamba Watanzania wengi wanaweza kuzimudu. 

Akiwa katika mahafali hayo, Sanga alijionea karakana na kushuhudia maonesho ya ujuzi na umahiri wa wanafunzi katika fani mbalimbali ikiwemo utengenezaji wa batiki, sabuni, uashi, ufundi seremala na ufundi wa magari.

Mahafali ya chuo cha VETA Makete ilihusisha wahitimu 64, miongoni mwao wavulana 52 na wasichana 12, katika fani za Ushonaji, Ufundi wa Magari, Useremala na Uashi.

No comments:

Post a Comment