CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Friday 30 November 2018

Wenye ulemavu waiomba VETA kuhuisha mitaala yake


Mratibu wa Idara ya Maendeleo Vijana na Chipukizi wa Chama cha Wasiiona Tanzania, Kiongo Itambu ameiomba Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kuhuisha mitaala yake ili iweze kuwa rafiki zaidi kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa watu wenye uelemavu wa aina zote hasa wasioona.

Itambu alisema hayo jana Novemba 29, 2018 wakati akipokea hundi ya Shilingi laki tano kutoka VETA kwa ajili ya kuwezesha kiongozi mmoja wa chama hicho kuhudhuria maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu itakayofanyika Desemba 1, 2018 mkoani Simiyu.

Alisema chama hicho kinatambua mchango wa VETA katika kuwapatia vijana ujuzi na kwamba watu wengi zaidi wenye ulemavu wakipata ujuzi huo utawasaidia kuinua uchumi wao na kuchangia pato la taifa.

“Tunaomba sana VETA iwaangalie kwa jicho la pili watu wenye ulemavu ili nao waweze kupata fursa zaidi ya kupata elimu ya ufundi stadi kwa kuandaa mitaala na mazingira rafiki ya kufundishia” Alisema

Aliishukuru VETA kwa msaada huo na kuomba Mamlaka hiyo iendelee kushirikiana nao kwa karibu katika shughuli mbalimbali wanazozifanya.

Naye Afisa Uhusiano wa VETA Dora Tesha alimsihi kiongozi huyo kutumia majukwaa mbalimbali na mikutano ya vyama vya wenye ulemavu kuwafahamisha watu hao juu ya fursa zilizopo katika vyuo vya Ufundi stadi nchini na kuwahamasisha kuzitumia vyema kupata ujuzi na kuweza kujiajiri wenyewe.

Alisema VETA imekuwa ikitoa mafunzo kwa watu wenye ulemavu ingawa idadi kubwa ya wanaojitokeza ni wenye ulemavu wa viungo ambapo kwa mwaka 2017 jumla ya vijana wenye ulemavu 334 walipata mafunzo katika fani mbalimbali katika vyuo vya ufundi stadi na kwamba kati yao 214 ni wenye ulemavu wa viungo na 11 pekee ndiyo wasiiona.

Alimuomba kiongozi huyo kuialika VETA kwenye makongamano na mikutano mbalimbali inayowakutanisha watu wenye ulemavu ili kuweza kutoa elimu juu ya fursa zilizopo katika vyuo vya Ufundi stadi na kufafanua hoja mbalimbali.

No comments:

Post a Comment