CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Wednesday 27 March 2024

WALIMU VETA WANOLEWA KUIMARISHA UTOAJI MAFUNZO SEKTA YA NGUO NA MAVAZI


Walimu 56 wa fani ya Ushonaji,  Ubunifu na Teknolojia ya Nguo kutoka  vyuo vya VETA nchini wamepatiwa mafunzo yenye lengo la kuwajengea uwezo katika kuboresha utoaji mafunzo, kufuatia mabadiliko ya mitaala katika fani hiyo.

 

Akifunga mafunzo hayo ya siku tatu yaliyofanyika katika ukumbi wa chuo cha VETA Dodoma, leo tarehe 27 Machi, 2024,  Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Antony Kasore amesema mabadiliko makubwa yamefanyika katika mitaala ya fani hiyo iliyohuishwa mwaka 2022, ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko la ajira.

“Kupitia mafunzo haya, tunatarajia mkawe mawakili wema katika kuhakikisha kwamba ufundishaji unaendana na mabadiliko mitaala na kasi mabadiliko makubwa ya teknolojia na mahitaji ya soko la ajira kwa ujumla” amesisitiza.

Sambamba na kuwajengea uwezo katika eneo la mafunzo, CPA Kasore ameahidi kuwa Mamlaka itafanya juhudi za kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo kuwapatia mashine na vifaa vya kisasa vyenye uwezo wa kubeba uhalisia wa mahitaji ya kasi ya mabadiliko ya teknolojia katika ufundishaji.

“wito wangu kwenu baada ya mafunzo haya na mara mtakapopokea vifaa na mashine hizo mtatusaidia kuwaandaa wanafunzi na wahitimu watakaotangaza ubora wa fursa ya mafunzo katika fani, hasa eneo la ubunifu, kujitangaza, kutafuta na kuchangamkia soko kupitia mitandao mbalimbali, pamoja na kuwashirikisha wataalamu kutoka nje ili wanafunzi wetu wahitimu wakiwa wenye tija zaidi”amesema

Akisoma risala kwa niaba ya walimu hao kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Bi.Winifrida Ndunguru kutoka chuo cha VETA-Dakawa amesema, Mafunzo hayo yamewawezesha kupitia changamoto zote zilizokuwa zikiwakabili hasa kwenye eneo la mitaala mipya na kuzipatia ufumbuzi wenye uwelewa wa pamoja,kujifunza mbinu mpya za kupakua mawasilisho kwa njia ya elektroniki, kutumia TEHAMA na mifumo ya mitandao mbalimbali itakayowawezesha kupata zana za kufundishia na kujifunzia kwa nadharia na vitendo na kuahidi utekelezaji wake mara watakaporejea vituoni mwao.


Nae Bi. Anna Nyoni aliemwakilisha Mkurugenzi wa mafunzo VETA Makao Makuu, amemshukuru Kaimu Mkurugenzi Mkuu, kwa kuruhusu na kuona haja ya kuwepo kwa mafunzo hayo ambayo yamefungua njia ya kutolewa kwa ufafanuzi wa mitaala ya kozi hiyo iliyohuishwa mwaka 2022 pamoja na utekelezaji wake.

Monday 25 March 2024

Watumishi VETA wapanda miti 40,000

Watumishi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) nchini wamepanda miti zaidi ya 40,000 ikiwa ni mwitikio wao kuelekea Maadhimisho ya miaka 60 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Akizungumza wakati wa zoezi la upandaji miti lililohusisha wafanyakazi wa VETA Makao Makuu, jijini Dodoma, leo tarehe 25 Machi, 2024, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema zoezi hilo limefanyika kwenye vituo vya VETA nchini ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali ya kila mwananchi na kila taasisi kupanda miti ili kutunza mazingira.

CPA Kasore amewaasa watumishi hao kutunza miti iliyopandwa ili ikue na kuleta maana halisi ya zoezi hilo na pia akawahimiza watumishi kuendelea na zoezi hilo katika maeneo wanayoishi.

 “Kupanda miti ni jambo moja na kutunza miti hiyo ni jambo lingine la muhimu sana…Nasisitiza tukatunze miti hii ili ikue na kutupa uhai pamoja na kuboresha muonekano wa mazingira yetu,” amesema.

CPA Kasore ameshukuru Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kutoa miti hiyo bure na kuahidi kuendeleza ushirikiano katika shughuli mbalimbali za uhifadhi wa misitu na utunzaji mazingira.

Afisa Misitu wa TFS Kanda ya Kati, Jenipha Elius, amesema anaamini miti hiyo itatunzwa na kukua vizuri hasa kwa kuzingatia kuwa imefuata hatua zote muhimu za kitaalamu za upandaji miti.

Amewasihi watumishi wa VETA kujenga utamaduni wa kupanda miti kwenye maeneo wanayoishi na kujipatia faida mbalimbali ikiwemo hali nzuri ya hewa pamoja na matunda na kuwakaribisha kupata miti bure kutoka TFS.

Furaha Paul ni miongoni mwa watumishi wa VETA Makao Makuu walioshiriki zoezi hilo ambaye amesema amejisikia fahari kupanda miti ambayo itanufaisha watanzania wengi kwa miaka mingi ijayo.

 “Kwa kweli najisikia furaha kushiriki kwenye zoezi hili la kihistoria kwa kuwa naamini miti hii itatumiwa na sisi, watoto wetu, wajukuu hadi vitukuu vyetu,”amesema

Kilele cha Maadhimisho ya Miaka 60 Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kinatarajiwa kuwa tarehe 26 Aprili, 2024.





Thursday 21 March 2024

KAMATI YA BUNGE YAPONGEZA UTOAJI MAFUNZO YA UANAGENZI CHUO CHA VETA MWANZA

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, imepongeza utoaji mafunzo ya uanagenzi katika chuo cha VETA Mwanza, kupitia ufadhili wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.

Pongezi hizo zimetolewa Jijini Mwanza, tarehe 19 Machi, 2024, wakati wa ziara ya Kamati hiyo kukagua utekelezaji wa mafunzo ya ukuzaji ujuzi kwa njia ya Uanagenzi katika chuo cha VETA Mwanza.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Fatuma Hassan Toufiq, amesema kazi kubwa ya kamati yake ni kuangalia na kukagua utekelezaji wa miradi ambayo Serikali imetoa fedha ili kuona thamani ya fedha katika miradi hiyo.

 “Katika chuo hiki tumefarijika sana kuona vijana mbalimbali wakipatiwa mafunzo…tumepita katika karakana tumejionea vijana wa kike na kiume wakijifunza namna ya kuwa mafundi wa aina mbalimbali kama vile mafundi bomba, mafundi umeme, useremala na wengine wengi,” amesema.

Wakiwa kwenye karakana za mafunzo, wajumbe hao waliwapongeza vijana kwa umahiri wa kuonesha na kuelezea kile walichojifunza na bidhaa mbalimbali walizozalisha kutokana na mafunzo.


Mhe. Toufiq amewataka vijana waliopata mafunzo ya kukuza ujuzi kwa njia ya uanagenzi katika chuo cha VETA Mwanza kuhakikisha wanatumia vyema ujuzi wao ili kuwaletea tija katika shughuli zinazohusiana na ufundi stadi, hivyo kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.

Amesema Kamati hiyo itaishauri Serikali kuona uwezekano wa kuwawezesha wahitimu wa programu hiyo vifaa vya kufanyia kazi ili waweze kujiajiri.

Naye Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja, amesema programu ya ukuzaji ujuzi kwa njia ya uanagenzi imelenga kuwezesha nguvukazi ya Taifa, hususani iliyopo katika soko la ajira, kupata ujuzi na stadi za kazi stahiki ili iweze kujiajiiri au kuajiriwa.

Amesema jumla ya shilingi bilioni 2.7 zimetengwa ili kuwezesha utekelezaji wa programu kwa vijana 6000 wakiwemo wenye ulemavu 84.

Katika chuo cha VETA Mwanza jumla ya wanafunzi 132 (wanaume 102 na wanawake 30) wanaendelea na mafunzo katika fani za Useremala, Uashi, Upakaji rangi, Ufundi Mashine za kuchakata Pamba, Ufundi Bomba, Umeme wa Majumbani, Ufundi Magari, Upishi na Uchomeleaji na Uungaji Vyuma.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Antony Kasore, VETA imeanzisha programu mbalimbali ambazo zinawasaidia wananchi wa Kitanzania kupata ujuzi na kufanya shughuli mbalimbali ambazo zitawaingizia kipato.

Baadhi ya vijana wanaopata mafunzo hayo, wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa kuwapatia fursa hiyo muhimu na kusema baada ya mafunzo hayo wanatarajia kujiajiri ili kuweza kujikimu katika maisha yao.

Aidha, wanafunzi hao wameiomba Serikali kuwasaidia vifaa vya kazi za ufundi stadi kwa fani mbalimbali walizojifunza ili utekelezaji wa shughuli hizo baada ya kuhitimu uweze kufanikiwa.



Wednesday 20 March 2024

362 WANUFAIKA NA MAFUNZO YA UANAGENZI KATIKA UFUNDI WA ZANA NA MITAMBO YA KILIMO

 

Jumla ya wanagenzi 362 (319 Me 43Ke) wamenufaika na mafunzo ya Uanagenzi Pacha kwenye fani ya Ufundi wa Zana na Mitambo ya Kilimo kupitia mradi uliotekelezwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Taasisi ya Kijerumani ya “West German Skills Craft (WHKT)” katika vyuo vitano (5) vya VETA vya Manyara, Kihonda, Dakawa, Arusha na Mpanda.


Hayo yamebainishwa, tarehe 19 Machi 2024 na Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi wa VETA, Abdallah Ngodu, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa VETA kwenye hafla ya kuhitimisha mradi huo iliyofanyika kwenye Chuo cha VETA cha Mkoa wa Manyara, kilichopo mjini Babati.

                                Mafunzo ya Uanagenzi hutolewa kwa utaratibu wa kupokezana wanafunzi (wanagenzi) kati ya vyuo na mahala pa kazi, ambapo katika mradi huo wanagenzi walikuwa wakihudhuria mafunzo kwenye karakana za vyuo kwa kipindi maalum, kisha kwenda kwenye mafunzo ya vitendo katika viwanda na mashamba ya kilimo. Mafunzo hayo hutolewa kwa kipindi cha miaka mitatu ambapo kwa kila mwaka wanagenzi wanatumia wiki 20 kwa mafunzo chuoni na wiki 32 kwa mafunzo ya sehemu ya kazi.

Ngodu ameyataja manufaa mengine yaliyopatikana kupitia mradi huo kuwa ni pamoja na walimu wa VETA kupatiwa mafunzo katika ngazi ya kitaifa na kimataifa ili kuwawezesha kutoa mafunzo bora yanayokidhi mahitaji ya makampuni na viwanda, pamoja na upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kilimo kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia.

Ameongeza kuwa wananchi wa mikoa vilivyopo vyuo vilivyotekeleza mradi wamepata fursa ya kujifunza juu ya matumizi na utunzaji wa zana na mitambo ya kilimo pamoja na mbinu za kuzuia upotevu wa mazao baada ya mavuno (Prevention of Post-harvest Losses).

Ameishukuru Serikali ya Ujerumani kwa kuwezesha utekelezaji wa mradi huo na kusisitiza kuwa VETA itaendelea kutumia mfumo huo kama mbinu mojawapo ya kutoa mafunzo katika vyuo vyake.

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Taasisi ya WHKT ya Ujerumani, Bastian Hermans amesema Ujerumani inajivunia kuanzisha mfumo huo hapa nchini na kwamba WHKT imefurahia mafanikio yaliyotokana na utekelezaji wa mradi huo.


Muasisi wa Mradi huo kwa upande wa Ujerumani, Herman Roeder ametoa wito kwa VETA kutumia vyema uzoefu walioupata katika utekelezaji wa mradi huo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2018 ili kuboresha zaidi utoaji mafunzo na kuzalisha vijana wenye ujuzi katika kutumia zana na mitambo ya kilimo.

Kwa upande wao wadau wa kilimo walionufaika na mradi huo wameishauri VETA kuendeleza na kupanua wigo wa utoaji wa mafunzo kwa mfumo huo ili kuzalisha nguvukazi kwa ajili ya kuhudumia sekta ya kilimo ambayo itasaidia kukuza na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao na kuchangia uchumi wa nchi.

Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Kilimo Tanzania na Mkurugenzi wa kampuni ya Kavel Coffee Plantation Ltd ya mkoani Manyara, Jitu Soni, amekiri kuwa mafunzo ya uanagenzi kwenye ufundi wa zana za kilimo yamewezesha makampuni ya kilimo kupata vijana wenye ujuzi wa kutumia na kuhudumia zana na mitambo ya kilimo na hivyo kuchangia kuongeza tija katika Sekta ya Kilimo.

“Kupitia mfumo huu tumepata vijana wazuri sana wenye utaalamu wa kuhudumia zana za kilimo na kufanya ukarabati wa vifaa vya kilimo na hivyo kutupa uhakika wa kuendesha shughuli zetu,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Oljoro Plantations Ltd ya Jijini Arusha, Ray Travas, ametoa wito kwa Serikali kuongeza wigo wa utoaji mafunzo kupitia mfumo huo ili kuihakikishia Sekta ya Kilimo upatikanaji wa nguvu kazi yenye utaalamu wa kutumia na kutunza zana na mitambo ya kilimo na kuongeza tija kwenye kilimo.

Mwakilishi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mjumbe wa Bodi ya VETA, Mhandisi Ezekiel Kunyaranyara, amesema Wizara itaendelea kuweka msisitizo na kuwezesha utoaji mafunzo kwenye Sekta ya Kilimo ili kuwezesha upatikanaji wa wataalamu mahiri watakaohudumia sekta hiyo kwa ufanisi na kuongeza tija.

Mhandisi Kunyaranyara ametoa wito kwa wahitimu wa VETA kujiunga kwenye vikundi na kuanzisha shughuli mbalimbali kulingana na fani walizosoma ili kuwawezesha kujipatia mikopo inayotolewa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya kuendeleza shughuli za uzalishaji.