CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Wednesday, 11 June 2025

VETA KUANZISHA KLABU ZA UBUNIFU KATIKA VYUO VYAKE

 

Kwa kutambua umuhimu wa Ubunifu kama nguzo muhimu katika kuboresha mafunzo ya ufundi stadi na mahitajio halisi ya soko la ajira, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), imepanga kuanzisha Klabu za Ubunifu katika vyuo vyake nchini.

Lengo la kuanzisha Klabu hizo ni kutaka kukuza uwezo wa wanafunzi na Wakufunzi katika utatuzi wa matatizo kwa njia ya kibunifu, kuendeleza mawazo mapya na kutumia maarifa yao kutatua changamoto za jamii kiuhalisia.

Katika kutekeleza mpango huu, VETA imeitisha kikao cha siku nne kuanzia tarehe 11 Juni, 2025 katika ukumbi wa Mt. Gaspar jijini Dodoma ikihusisha wadau muhimu katika maendeleo ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ili kuwasilisha mpango wa kuanzisha Klabu, kubadilishana uzoefu na kuandaa mpango kazi wa utekelezaji.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA. Anthony Kasore amesema, katika dunia ya sasa ubunifu ni kitu cha lazima ili kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii hivyo kuna haja ya kuwajengea watu uwezo wa kibunifu.

Amesema, kupitia Klabu za Ubunifu, vijana watachochewa kubuni, kuwa wajasiriamali, kusimamia bunifu zao katika kukuza na kuchochea maendeleo yao binafsi kwa kuanzisha viwanda vya kuzalisha bidhaa za ndani badala ya kutegemea kutoka nje.

Amesema, sambamba na mpango wa Klabu za Ubunifu,  VETA imeanzisha kampuni ambayo itaingia makubaliano na wabunifu mbalimbali wanaozalisha bidhaa ili kuzizalisha kwa wingi na kuziusa  na kuziuza.

CPA. Kasore ameongeza kuwa, kila mwaka zaidi ya vijana zaidi ya elfu sitini (60,000) wanapata mafunzo katika vyuo vya VETA nchini, hivyo kuna haja ya kuwajenga uwezo na kuwatengenezea mazingira wezeshi ya kiubunifu ili waweze kuzalisha bidhaa kulingana na mahitaji ya jamii husika.

MRADI WA INCLU-CITIES KUNUFAISHA VIJANA 350 TANGA

 

Vijana 350 wanatarajiwa kunufaika na mafunzo ya Ufundi Stadi katika chuo cha VETA-Tanga kama sehemu ya kukiandaa chuo hicho kuwa kitovu cha umahiri katika utoaji mafunzo ya ufundi stadi nchini.

Vijana hao wanatarajiwa kupata mafunzo hayo kupitia mradi wa INCLU-CITIES unaotekelezwa na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ubelgiji (ENABEL) wakishirikiana na chuo cha VETA-Tanga.

Tarehe 10 Juni, 2025 katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha VETA cha mkoa wa Tanga.

Akizindua mradi huo kupitia kikao kazi cha wadau leo, tarehe 10 Juni 2025, Mkuu wa mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt.Batilda Salha Buriani ameipongeza VETA kwa kuendelea kuwaandaa vijana kuwa na ujuzi bora wa kuweza kuajiriwa au kujiajiri katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayopatikana na inayoanzishwa katika jiji la Tanga.

  “tunaishukuru VETA kwa kushirikiana na ENABEL kuzindua na kukubali kutekeleza mradi huu ambao kupitia mafunzo yatakayotolewa tutawakomboa vijana kwa kuwapa maarifa ya jinsi ya kumudu mazingira yao,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha VETA Tanga, Gideon Ole Lairumbe amesema kuwa vijana hao 350 watatoka katika kata mbalimbali za mkoa wa Tanga ambapo vijana 150 watakuwa wale ambao hawakuwahi kuwa na ujuzi wowote, 150 ni wenye ujuzi katika sekta mbalimbali, lakini wana mapungufu kadha wa kadha katika utendaji wao, hivyo watapatiwa mafunzo yatakayowasaidia kurekebisha mapungufu hayo.

Ameongeza kuwa 50 ni wale ambao wamepata mafunzo nje ya mfumo rasmi wa utoaji mafunzo, hivyo watafanyiwa tathmini na kurasimishiwa ujuzi wao.

Mratibu wa Mafunzo kutoka Mradi wa INCLU-CITIES Bw. Thomas Kakurwa amesema mbali na kutoa Mafunzo kwa vijana hao 350, mradi huo utasaidia kuwajengea uwezo walimu watakaofundisha katika fani husika ambazo ni Uandaji wa chakula, Uvuvi, Umeme jua, Uungaji na uundaji vyuma, matengenezo ya pikipiki za umeme na simu za mkononi pamoja na kuboresha na kununua vifaa vya kufundishia katika karakana.

Mradi wa INCLU-CITIES umekwishaanza kutekelezwa kwa hatua za awali katika mikoa ya Tanga, Mwanza na Pemba kutoka Aprili, 2025 na unatarajiwa kukamilika Septemba, 2026.