Mafundi wa stadi mbalimbali mkoani Mbeya wametakiwa kuendelea kujiongezea ujuzi na kufanya kazi zao kwa uadilifu na uaminifu ili kujijengea imani kwa wateja na kujiinua kiuchumi.
Wito huo umetolewa leo, tarehe 29 Aprili 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mheshimiwa Beno Malisa, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mheshimiwa Juma Homera, katika Kongamano la Mafundi lililofanyika katika ukumbi wa Tughimbe, Mafiati, jijini Mbeya.
Akizungumza katika katika Kongamano hilo lililoandaliwa na kampuni ya Fundi Smart kwa kushirikiana na VETA, Malisa amewataka mafundi kuchangamkia mafunzo yanayotolewa na VETA ili kuongeza ujuzi na kuendana na mabadiliko ya teknolojia kwa kadri ya muda.
"Nendeni mkapate ujuzi ambao utawasaidia kufanya kazi zenu kwa ufanisi zaidi. Pia fanyeni kazi kwa uaminifu. Kama tunavyojua, uaminifu ni msingi wa mafanikio kwani wateja na jamii watawaamini na kuwapatia kazi zaidi ikiwa mtakuwa waaminifu kwao" amesema Malisa.
Aidha, Malisa amewakumbusha mafundi umuhimu wa kutumia vifaa vya usalama wawapo kazini ili kulinda afya na maisha yao.
"Ni muhimu mzingatie matumizi ya vifaa vya kujikinga wakati mnapotekeleza majukumu yenu, ili muwe salama muda wote wa kazi," ameongeza.
Vilevile, Malisa amewahimiza kuunda umoja na kufanya kazi kwa ushirikiano, kwani pia utaiwezesha Serikali kuwafikia kwa urahisi katika kuwahudumia na kuwawezesha kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, ametumia jukwaa hilo kuelezea fursa ya mafundi waliopata ujuzi nje ya mfumo rasmi wa mafunzo kurasimisha ujuzi wao kupitia VETA.
"Kila mwenye ujuzi alioupata nje ya mfumo rasmi anakaribishwa VETA ili urasimishwe na apate cheti kinachotambulika rasmi, ambacho kitamwezesha kujiongezea fursa za kazi, ikiwemo kushiriki kikamilifu katika miradi ya maendeleo ya Serikali," amesema CPA Kasore.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Fundi Smart, Fredy Pole, ameishukuru VETA kwa kushirikiana na kampuni yake katika kurasimisha ujuzi wa mafundi, akisema mpango huo utachochea tija katika sekta ya ufundi.
“Lengo letu ni kuwaunganisha mafundi na fursa za biashara, viwanda, wateja pamoja na taasisi za kifedha ili waweze kunufaika zaidi na kazi zao,” amesema Pole.
Kongamano hilo la
Mafundi mkoani Mbeya limewakutanisha mafundi takribani zaidi ya 1000 kutoka
fani mbalimbali zikiwemo useremala, uashi, uchomeleaji, uungaji na uundaji
vyuma, ufundi simu, umeme, uchoraji, na upasuaji miti.