Serikali kupitia Mamlaka ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeanza utekelezaji wa ujenzi wa Vyuo vya Elimu
na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa Mikoa ya Geita, Njombe, Rukwa na Simiyu ikiwa ni
sehemu ya kutoa huduma ya ufundi na ujuzi ili kukidhi mahitaji ya mikoa hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya
kukabidhi maeneo ya ujenzi wa vyuo vya mkoa wa Geita na Wilaya ya Chato,
Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Peter Maduki alisema
ujenzi wa vyuo hivyo kwa mikoa hiyo una lengo la kutekeleza mkakati wa Mamlaka
wa kuongeza udahili hadi kufikia idadi ya wanafunzi 700,000 ifikapo mwaka 2020.
Alisema kuwa jitihada hizo zinaenda
sanjari na utekelezaji wa nia njema ya Serikali ya awamu ya tano ya kuhakikisha
kuwa vijana wanapata ujuzi stahiki utakaowawezesha kuajiriwa au kujiajiri ili
kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi na kuhakikisha nchi inafikia uchumi
wa kati ifikapo 2025.
Akikabidhi rasmi nyaraka za ujenzi wa
Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) cha Mkoa wa Geita chenye
ukubwa wa hekta 27 kwa Mkandarasi anayejenga chuo hicho Kampuni ya Kitanzania
Skywards Construction
mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel, Maduki alisema kuwa gharama ya ujenzi wa chuo hicho ni kiasi cha Sh bilioni 9.9 fedha za mkopo kutoka benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel, Maduki alisema kuwa gharama ya ujenzi wa chuo hicho ni kiasi cha Sh bilioni 9.9 fedha za mkopo kutoka benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Kwa upande wa chuo cha Wilaya ya Chato,
alisema ujenzi wake utagharimu kiasi cha Sh bilioni 10.7 ambazo ni fedha za
ndani na ujenzi utafanywa na kampuni ya Kitanzania ya C.F Builders yenye makao
yake jijini Mwanza.
Alisema vyuo hivyo vitakapokamilika
vitakuwa na uwezo wa kudahili jumla ya wanafunzi 2940, ambapo kwa chuo cha mkoa
wa Geita pekee kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 660 kwa ngazi tatu kwa
mafunzo ya muda mrefu kwa mwaka na wanafunzi wasiopungua 1000 kwa mafunzo ya
muda mfupi huku Chuo cha VETA Chato chenye ukubwa wa ekari 70 kitakuwa na uwezo
wa kudahili wanafunzi 480 kwa ngazi hizo tatu za mafunzo ya muda mrefu na
wanafunzi wasiopungua 800 kwa mafunzo ya muda mfupi.
Alizitaja baadhi ya fani zitakazotolewa
katika vyuo hivyo kuwa ni pamoja na Ufundi wa Mitambo Mizito, Ufundi
Elektroniki, Mechatronic,Ufundi Umeme wa Magari,Ufundi Uashi,Ufundi Umeme,
Ufundi bomba, Ukarimu na Usindikaji wa Samaki,Useremala, Mafunzo ya Uhazili na
Compyuta na Ufundi wa vifaa tiba.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita
Mhandisi Robert Gabriel alimshukuru Rais John Magufuli kwa kazi kubwa
anayofanya ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali nchini sambamba na ujenzi wa
vyuo hivyo vya kisasa ambavyo vitawawezesha wananchi hasa vijana kupata ujuzi
ili waweze kujiajiri sanjari na kuwavutia wawekezaji kwenda kuwekeza mkoani
kwake.
Aliushauri uongozi wa VETA kutoa
kipaumbele kwa fani zinazohusiana na teknolojia ya uchimbaji ili kuwawezesha
wachimbaji wadogo kuchimba madini kitaalam na kuongeza tija katika shughuli
hiyo inayofanywa na vijana wengi mkoani Geita.
Aliwataka wakandarasi wa miradi hiyo
kuhakikisha kuwa wanakamilisha kazi ya ujenzi kwa muda uliopangwa kwa kuwa
wananchi wa mkoa wa Geita wana matarajio makubwa ya kuona miradi hiyo
inakamilika kwa wakati mwafaka na kwa ubora unaotarajiwa.
“Nitakuwa nakagua ujenzi wa miradi hii
mara kwa mara ili kuona utekelezaji wake”, alisema.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkuu wa
Wilaya ya Chato Elias Makori aliishukuru serikali kwa kuamua kujenga chuo hicho
wilayani Chato ambacho alisema kitaongeza ajira, ujuzi kwa vijana sanjari na
kupunguza umaskini
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Wilaya ya Chato Batholomeo Manunga alisema ujio wa mradi wa ujenzi wa chuo
hicho utatatua changamoto ya ajira kwa vijana ambao watapata ujuzi
utakaowawezesha kuajiriwa na kujiajiri na kukuza vipato vyao.
No comments:
Post a Comment