CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Monday 1 October 2018

Waziri Mkuu avutiwa na mafunzo ya VETA katika sekta ya madini


Waziri Mkuu wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa amevutiwa na mafunzo yanayotolewa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kusaidia sekta ya madini.

Waziri Mkuu alibainisha kuvutiwa kwake na kushangazwa na umahiri wa wanafunzi wa VETA baada ya kutembelea banda la VETA tarehe 30 Septemba, 2018 katika maonesho ya Teknolojia ya Uchimbaji na Uwekezaji kwenye Madini ya Dhahabu yaliyokuwa yakifanyika katika viwanja vya Kalangalala, mjini Geita kuanzia tarehe 24 hadi 30 Septemba, 2018.

Akitembelea mabanda kabla ya kufunga rasmi maonesho hayo, Waziri Mkuu alipita banda la VETA na kupata maelezo kutoka kwa Meneja Uhusiano wa VETA, Sitta Peter juu ya mafunzo mbalimbali yanayotolewa na VETA yanayogusa sekta ya madini ikiwa ni pamoja na ufundi wa mitambo mikubwa, uendeshaji mitambo mikubwa, ulipuaji wa miamba na ukataji na ung’arishaji madini ya vito, kisha kujionea umahiri wa wanafunzi wa VETA katika stadi mbalimbali.

Miongoni mwa yaliyomvutia zaidi ni ustadi aliouonesha mwanafunzi wa VETA Shinyanga katika fani ya Ukataji na Ung’arishaji Madini ya Vito, Jesca Jonathani Nkani alipokuwa akionesha namna ukataji na ung’arisha madini unavyofanyika, pamoja na ujuzi wa uendeshaji mitambo mikubwa uliooneshwa na mwanafunzi wa VETA Moshi katika programu Mafunzo ya Ufundi kwa Ajili ya Uchimbaji Madini (IMTT), Careeen Vedasto.

Pamoja na kueleza kufurahishwa kwake wakati akiwa katika banda la VETA, Waziri Mkuu alibainisha pia katika hotuba yake ya ufungaji ambapo licha ya kuipongeza VETA kwa kuanzisha mafunzo hayo, aliwahamasisha wananchi, hususani vijana kujifunza ujuzi huo ambao unapatikana nchini.

Alisema, kwa muda mrefu imekuwa ikidhaniwa kuwa teknolojia ya ukataji na ung’arishaji madini inapatikana nje ya nchi tu na wale wanaoiendesha hapa nchini ni wageni tu, kumbe ujuzi huo sasa unatolewa katika vyuo vya hapa nchini na kwamba Watanzania wanaweza kujifunza na kuendesha shughuli za kuongezea thamani madini hapahapa nchini.

“Nilivutiwa sana na yule binti alivyokuwa aking’arisha madini kwa ustadi, nilitamani ninunue moja, lakini alinieleza hizo ni kwa ajili ya mafunzo…………” alisema.

Aliwaasa wananchi kutumia mafunzo mbalimbali yanayotolewa na VETA ili kuongeza tija katika uchimbaji na uchakataji wa madini.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Angela Kairuki alieleza kuwa Wizara yake itawasiliana na VETA na Kituo cha Utambuzi na Ukataji Madini ya Vito (TGC) kuona ni namna kuweza kuwa na ushirikiano na kusaidiana katika eneo la utambuzi, ukataji na ung’arishaji madini ya vito.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko aliiomba VETA kupunguza wasiwasi wa wahitimu wa kozi ya Ukataji na Ung’arishaji madini juu ya suala la kupata ajira kwa kuwa sheria na taratibu zilizowekwa na serikali sasa zinawabana wawekezaji, kiasi kwamba watalazimika kuajiri wahitimu wengi wa hapa nchini.

“ili upate dealer license (leseni ya uwakala), unapaswa uwe na mashine zisizopungua 30 na wataalam wa kuzitumia hizo mashine, na utaalam tunaoutaka ni ule wa mtu aliyefuzu na cheti ndo uthibitisho. Sasa hawa wataalam watawapata wapi kama si kutoka kwenu VETA?,” alisema na kuhoji.
  

No comments:

Post a Comment