CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Tuesday 27 November 2018

VETA-Njiro kuanzisha mafunzo ya utalii


Chuo cha VETA cha Hoteli na Utalii (VHTTI)-Njiro, kilichopo jijini Arusha kiko mbioni kuanzisha mafunzo ya utalii kwa ngazi ya stashahada na astashahada sambamba na mafunzo yanayohusiana na mambo ya hoteli ambayo yamekuwa yakitolewa tangu kuanzishwa kwa chuo mwaka 2011.

Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Chuo hicho, Christopher Ayo wakati wa mahafali ya sita ya chuo hicho yaliyofanyika Novemba 23 mwaka huu chuoni hapo yakiwahusisha wahitimu jumla ya wahitimu 416 wakiwemo wanaume 122 na wanawake 294 wa mahafali ya pili (2014), ya tatu (2015), ya nne (2016) ya tano (2017) na ya Sita (2018).

Alizitaja kozi ambazo ziko mbioni kuanzishwa kuwa ni Uongozaji wa Watalii na yale ya Uendeshaji na Utoaji Huduma za Kitalii na Usafiri na kusema kuwa zimeandaliwa kwa ushirikiano na chuo cha Nova Scotia Community College cha nchini Canada chini ya mradi wa ISTEP.

“Tayari mitaala imetengenezwa na iko kwenye hatua za mwisho kupitishwa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi-NACTE,” alisema.

Sambamba na mpango huo, Ayo alisema kuwa chuo hicho pia kina mpango wa kuongeza udahili kutoka 220 hadi kufikia 500 kwa mwaka kwa kozi zote yaani usimamizi wa hoteli na utalii.

Vilevile, chuo kina mpango wa kuanzisha masomo kwa njia ya mtandao (E-learning) hasa kwa wahitaji walio mbali na chuo wanaotaka kujiendeleza.

Ayo aliwahamasisha wahitimu kujenga moyo wa kujiajiri ili kuweza kuzalisha na kuajiri wengine hasa ukizingatia kuwa pamoja na kupata mafunzo katika fani zao walifundishwa pia ujasiriamali na namna ya kutafuta masoko ya bidhaa au huduma kwa wateja.

Chuo cha VETA cha Hoteli na Utalii (VHTTI)-Njiro kilianzishwa mwaka 2011 kikiwa kinatoa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi katika fani za Mapokezi (Front Office Operation); Upishi (Food Production); Huduma na Mauzo ya Vinywaji na Chakula (Food and Beverage Services and Sales); Utunzaji, Usafi wa Nyumba na Udobi (House Keeping and Laundry Services:

Baada ya kupata usajili wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), kozi zilihuishwa na kuwa tatu yaani mapokezi na Huduma za Malazi (Rooms Division); Huduma na Mauzo ya Chakula na Vinywaji (Food and Beverage Services and Sales) pamoja na Sanaa ya Uandaaji chakula na Mapishi (Culinary Art).

Chuo hicho pia kinatoa mafunzo ya muda mfupi katika fani mbalimbali kama Upambaji, Usafi wa majengo na maeneo ya wazi, Upishi, Huduma ya uuzaji vinywaji, uandaaji wa keki na upambaji na mafunzo ya uongozaji watalii.

Vilevile, Chuo kina hoteli ya kisasa yenye hadhi ya nyota tatu (Three Stars Hotel) iliyojengwa mahsusi kwa ajili ya mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi.

No comments:

Post a Comment