CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Tuesday 27 November 2018

VETA-Njiro yashauriwa kubuni kozi fupi kunufaisha wananchi wengi



Viongozi wa Chuo cha VETA Cha Hoteli na Utalii-Njiro (VHTTI) wameshauriwa kubuni kozi nyingi za muda mfupi katika nyanja za hoteli na utalii ili kunufaisha wananchi wengi zaidi.

Ushauri huo umetolewa Ijumaa tarehe 23 Novemba 2018 na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqarro katika mahafali ya sita ya VHTTI yaliyofanyika chuoni hapo yakihusisha jumla ya wahitimu 416 wakiwemo wanaume 122 na wanawake 294 wa mahafali ya pili (2014), ya tatu (2015), ya nne (2016) ya tano (2017) na ya Sita (2018).

Daqarro alisema kuwa nyanja za hoteli na utalii bado zina uhitaji mkubwa wa nguvukazi nchini hasa katika miji yenye shughuli nyingi za kiutalii kama Arusha na maeneo ya jirani, hivyo kozi za muda mfupi zinaweza kusaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa watu wenye ujuzi katika nyanja hizo.

“Kupitia mafunzo ya muda mfupi chuo kitaweza kugusa na kubadilisha maisha ya wananchi wengi ndani ya muda mfupi hususani kwa wananchi wetu wa jiji la Arusha na maeneo jirani,” alisema.

Aliongeza kuwa kutokana na Jumuiya ya Afrika Mashariki kuimarika kuna changamoto kubwa ya kupanuka kwa wigo wa uwanja wa ajira kufuatia kufunguliwa kwa mipaka baina ya nchi wanachama hivyo  kuna fursa pia katika nchi za jirani ingawa pia wataalamu kutoka nchi jirani wana fursa ya kuja kufanya kazi nchini.

Daqarro alieleza kufurahishwa kwake na takwimu za kuajirika kwa wahitimu wa chuo hicho ambapo alipewa taarifa kuwa asilimia 94 ya wahitimu hao wameshapata ajira na kwamba huo ni ushahidi wa ubora wa mafunzo yanayotolewa na chuo hicho.

Awali akitoa taarifa ya maendeleo ya chuo, Mkuu wa chuo hicho, Christopher Ayo alisema kuwa chuo hicho pia kina mpango wa kuongeza udahili kutoka 220 hadi kufikia 500 kwa mwaka kwa kozi zote yaani usimamizi wa hoteli na utalii. Vilevile, chuo kina mpango wa kuanzisha masomo kwa njia ya mtandao (E-learning) hasa kwa wahitaji walio mbali na chuo wanaotaka kujiendeleza.

Chuo cha VETA cha Hoteli na Utalii (VHTTI)-Njiro kilianzishwa mwaka 2011 kikiwa kinatoa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi katika fani za Mapokezi (Front Office Operation); Upishi (Food Production); Huduma na Mauzo ya Vinywaji na Chakula (Food and Beverage Services and Sales); Utunzaji, Usafi wa Nyumba na Udobi (House Keeping and Laundry Services:
Baada ya kupata usajili wa Baraza la Taifa la  Elimu ya Ufundi (NACTE) kozi zilihuishwa na kuwa tatu yaani mapokezi na Huduma za Malazi (Rooms Division); Huduma na Mauzo ya Chakula na Vinywaji (Food and Beverage Services and Sales) pamoja na Sanaa ya Uandaaji chakula na Mapishi (Culinary Art).

Chuo hicho pia kinatoa mafunzo ya muda mfupi katika fani mbalimbali kama Upambaji, Usafi wa majengo na maeneo ya wazi, Upishi, Huduma ya uuzaji vinywaji, uandaaji wa keki na upambaji na mafunzo ya uongozaji watalii.

Vilevile, Chuo kina hoteli ya kisasa yenye hadhi ya nyota tatu (Three Stars Hotel) iliyojengwa mahsusi kwa ajili ya mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi.

No comments:

Post a Comment