Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu amezindua Baraza la Wafanyakazi wa VETA Makao Makuu na kusisitiza uwajibikaji na mshikamano kama nguzo kuu ya mafanikio mahala pa kazi.
Akizungumza wakati wa
ufunguzi wa Baraza hilo katika ofisi za VETA Makao Makuu tarehe 6 Novemba 2020,
Dkt Bujulu amesema Baraza la Wafanyakazi ndilo jukwaa la kisheria la
majadiliano ya pamoja kati ya viongozi na watumishi kuhusu wajibu na maslahi ya
watumishi, hivyo likitumika vizuri litasaidia
kupunguza au kuondoa kabisa malalamiko ya wafanyakazi mahali pa kazi.
Aidha, amewataka
viongozi wote kutoa ushirikiano mkubwa kwa watumishi wanaowaongoza na
kuhakikisha masuala yote ya maendeleo na changamoto za wafanyakazi
zinashughulikiwa kwa wakati ili kuleta ufanisi, tija na kudumisha nidhamu
kazini na hivyo kuongeza ari ya wafanyakazi.
Dkt Bujulu
amesisitiza watumishi wa VETA kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kujituma kwa kuwa wana mchango mkubwa katika kufikia
malengo ya Serikali ya awamu ya tano ya ujenzi wa viwanda na uchumi.
Baraza la Wafanyakazi
wa VETA Makao Makuu liliundwa tarehe 5 Novemba 2020, ikiwa ni sehemu ya
mchakato wa Uundaji wa Mabaraza ya Wafanyakazi wa VETA.
No comments:
Post a Comment