Naibu Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, Mhe.
Abdallah Ulega (Mb), amefanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu
na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Dkt. Pancras Bujulu, na kumuelezea juu ya
mpango wake wa kujenga karakana za mafunzo ya ufundi stadi Wilayani Mkuranga.
Katika mazungumzo
hayo yaliyofanyika leo, tarehe 23 Desemba, 2020, katika ofisi za Makao Makuu ya
VETA jijini Dar es Salaam, Mhe. Ulega amemuarifu Mkurugenzi Mkuu wa VETA juu ya
mpango huo, ambapo analenga kushirikiana na wadau mbalimbali kujenga karakana
za ufundi stadi Jimboni kwake ili kuwezesha vijana kujipatia ujuzi wa kuendesha
shughuli mbalimbali za kichumi kwa ufanisi.
Mhe. Ulega ameiomba
VETA kumpa ushirikiano katika mpango huo, kwa kumpa mwongozo juu ya vigezo na
viwango vya karakana, vifaa, zana na mitambo ya kufundishia ili ujuzi
watakaoupata vijana hao uwawezeshe kupata vyeti vya VETA na kutambuliwa rasmi
kama mafundi stadi.
Mhe. Ulega
anadhamiria kujenga karakana za fani mbalimbali, zikiwemo za Ufundi Umeme,
Useremala, Uashi, Ufundi bomba na Uchomeleaji vyuma, hasa kwa kuzingatia kuwa
fani hizo ndio zinaongoza kwa wingi wa fursa za ajira kwa vijana wengi Jimboni
mwake.
Mkurugenzi Mkuu wa
VETA, Dkt. Pancras Bujulu, amesema VETA imepokea ombi la Mhe. Ulega kwa uzito
mkubwa na kwamba VETA itahakikisha inafanyia kazi ombi hilo na kulipa
kipaumbele ili vijana wa Mkuranga waweze kupata ujuzi na kufanya shughuli zao
kwa weledi.
Mkurugenzi Mkuu
ameshauri kuwa mafunzo kwa vijana hao yatolewe kwa mfumo wa Uanagenzi Pacha
(Dual-Apprenticeship System, DATS), na hivyo amekiagiza Kitengo cha DATS cha
VETA Makao Makuu kushirikiana naye katika kufanikisha azma yake hiyo.
Dkt. Bujulu
amempongeza Mhe. Ulega kwa kutambua umuhimu wa mafunzo ya ufundi stadi na
mchango wake katika kuwezesha vijana kujiajiri na kuleta maendeleo nchini.
No comments:
Post a Comment