Jumla ya vijana 4,000
wa mikoa ya Dodoma, Lindi na Manyara wanatarajia kunufaika na mafunzo maalum ya
ufundi stadi yatakayowapa ujuzi na
utayari wa kuajiriwa au kujiajiri, kupitia mradi wa Ajira na Ujuzi kwa
Maendeleo ya Tanzania, kwa kiingereza “Employment and Skills for Development
Tanzania”.
Makubaliano ya
utekelezaji wa mradi huo yametiwa saini tarehe 28 Juni 2021, jijini Dar es
Salaam kati ya Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu na Mkurugenzi Mkazi
wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Korea (KOICA) nchini Tanzania, Kyucheol
Eo.
Akizungumza wakati wa
kutia saini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkazi wa KOICA nchini Tanzania,
Kyucheol Eo, amesema kuwa Serikali yake imetenga kiasi cha Dola za
Kimarekani 5,300,000 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo na kwamba
utatekelezwa kwa miaka mitatu kuanzia 2021 hadi 2023.
Amesema VETA
itashirikiana kwa karibu na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani
(GIZ) katika utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha vijana wa kitanzania
wananufaika na ukuaji wa uchumi katika sekta zinazotegemea ujuzi wa ufundi
stadi.
“KOICA inafurahi
kushirikiana na VETA kusaidia vijana nchini Tanzania kupata ajira ikiwa ni
pamoja na kujiajiri ili waweze kutimiza ndoto zao. Tutashirikiana pia na GIZ
kutekeleza mradi huu ambao utanufaisha moja kwa moja vijana 4,000, ambapo kati
yao 1,400 ni wanawake,” amesema Mkurugenzi Mkazi wa KOICA nchini Tanzania,
Kyucheol Eo.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, ameishukuru Serikali ya Korea kwa
ufadhili huo na kusema kuwa mradi huo umejikita katika kutoa mafunzo ya muda
mfupi kwenye fani za Uchomeleaji (Welding), Ufundi Bomba wa Viwandani
(Industrial Plumbing) na Mekatroniki (Mechatronics).
Amesema mradi huo,
pamoja na mambo mengine, utawapatia vijana hao mafunzo ya ujasiriamali na kutoa
fedha kama mtaji ili kuwawezesha wahitimu kuanzisha miradi yao na kuwawezesha
kujiajiri. Mitaji hiyo itatolewa kwa timu za wanafunzi zitakazoshinda kupitia
uwasilishaji wa miradi bora itakayopatikana kupitia shindano maalum la
ujasiriamali litakalofanyika kila mwaka.
“Tuko tayari kutoa
mafunzo kwa vijana hao 4,000 waliolengwa na mradi huu ambao tunaamini kuwa
wakihitimu watakuwa na ujuzi utakaowawezesha kujipatia ajira na hasa kwa
kuzingatia uwepo wa miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa nchini
inayotoa fursa za ajira kwa vijana wengi wenye ujuzi,” Dkt. Bujulu amefafanua
zaidi.
Katika mradi huo,
KOICA pia itawezesha utoaji mafunzo kwa walimu wa ufundi stadi kwenye fani
zitakazohusika, kufanya mapitio ya mitaala iliyopo na kutengeneza mipya pamoja
na ununuzi wa mitambo na vifaa vya mafunzo.
No comments:
Post a Comment