CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Thursday 2 December 2021

Waziri Mkuu Majaliwa asisitiza ufundi stadi kuwezesha ajira kwa Watanzania

 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imejipanga kuwapatia ujuzi Watanzania kupitia mafunzo ya ufundi stadi ili waweze kujiajiri na kuajiriwa.

Akizungumza wakati wa kukagua na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa chuo cha ufundi stadi cha Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya leo tarehe 29 Novemba, 2021, Mhe. Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imefanya uamuzi wa kujenga vyuo vya ufundi stadi nchini ili wananchi hususani vijana wapate ujuzi na ufundi wa aina mbalimbali na kuweza kushiriki shughuli za kiuchumi na kujipatia kipato.

“Tumefanya maamuzi ya kujenga vyuo vya ufundi stadi VETA ili tupate vijana wa Kitanzania wa ngazi mbalimbali kitaaluma waje hapa wajifunze ufundi akirudi anaweza kuanzisha karakana yake akafanya kazi na kupata kipato… anaweza pia kuajiriwa na wenye karakana zenye ufundi huo.” amesema

Mhe. Majaliwa ameagiza ujenzi wa Chuo cha VETA Chunya ukamilike kwa wakati ili malengo ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya ufundi chuoni hapo yanafikiwa huku akiwataka wananchi kuendelea kuwa na imani na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omari Kipanga, amesema kwa sasa Serikali inajenga vyuo vya VETA kwenye Wilaya 29 ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi bilioni 48.8 zimeshatumika  kwa ajili ya ujenzi wa vyuo hivyo.

Mhe. Kipanga amesema kiasi kingine cha shilingi bilioni 64 kimetolewa na Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyuo hivyo pamoja na kuwezesha ujenzi wa vyuo vingine vinne vya mikoa ya Geita, Simiyu, Rukwa na Njombe.

Amemuhakikishia Mhe. Waziri Mkuu kuwa Wizara yake itasimamia miradi hiyo kwa weledi na uaminifu mkubwa ili kuhakikisha kiu ya watanzania ya kupata ufundi katika maeneo ya karibu inapatikana na kwamba chuo hicho kitakamilika ifikapo mwezi Februari, 2022.

Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu amesema ujenzi wa chuo hicho ulianza mwezi Machi, 2020 na kwamba mradi huo una jumla ya majengo 17 ambayo ni jengo la utawala, karakana nne, jengo la madarasa, mabweni mawili, bwalo la chakula, majengo matatu ya vyoo, nyumba ya mkuu wa chuo, nyumba ya familia mbili za watumishi, jengo la mitambo ya umeme, jengo la stoo na jengo la walinzi.

Dkt. Bujulu amesema chuo hicho kitakapokamilika kinatarajiwa kudahili wanafunzi 720 kwa mwaka katika fani za uhazili na kompyuta, ushonaji na ubunifu wa mitindo, uashi, umeme wa majumbani, ufundi magari pamoja na uchomeleaji na uungaji wa vyuma.


Kwa mujibu wa Dkt. Bujulu, hadi kukamilika jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 2.5 zinatarajiwa kutumika ambapo hadi sasa shilingi bilioni 1.6 zimeshatumika.

No comments:

Post a Comment