Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Francis Michael, amewataka watendaji wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kuhakikisha mwelekeo na kipaumbele cha utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi iwe ni kuwawezesha vijana kujiajiri, badala ya kutegemea kuajiriwa.
Dkt. Michael ameyasema hayo, tarehe 21 Septemba, 2022, jijini Dodoma alipofanya ziara Makao Makuu ya VETA ikiwa ni mwendelezo wa ziara za kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara yake kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hizo.
Dkt. Michael amesema kuwa Serikali imeweka kipaumbele kikubwa kwenye elimu ya ufundi stadi kwa kuwa ndilo eneo linaloweza kuwapatia vijana wengi ujuzi na maarifa ya kuwawezesha kutumia fursa zilizopo kujiajiri na kuendesha maisha yao.
“Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) ametupa kipaumbele sana sisi VETA, kwa sababu elimu anayoitilia mkazo Mheshimiwa Rais ni elimu ya umahiri (Competence-Based) ambayo imeanzia VETA. Mheshimiwa Rais anataka tunapowafundisha vijana wawe na elimu, ujuzi, maarifa, waweze kujiamini na kujiajiri,” amesema.
Ameongeza kuwa mitaala ikiandaliwa na mafunzo kutolewa kwa kipaumbele cha kujiajiri, kuna fursa nyingi zipo katika jamii ambazo vijana wanaweza kuzitumia baada ya kuhitimu.
“Mitaala iweze kuandaliwa katika namna ambayo
kijana akitoka VETA, hata akiambiwa nataka kukuajiri aseme hapana, mimi
nakwenda kujiajiri. Kuna fursa nyingi sana huko nje,” ameongeza.
Aidha Dkt. Michael
amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kupanua wigo wa
upatikanaji wa mafunzo ya ufundi stadi ambapo kwa sasa kazi kubwa ya ujenzi wa
vyuo vya ufundi stadi kila Wilaya inaendelea ili kuhakikisha vijana wa
kitanzania wanapata fursa ya kupata ujuzi wa kufanya kazi mbalimbali.
Awali akitoa taarifa ya utendaji kwa Katibu Mkuu, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, ameeleza kuwa miongoni mwa mafanikio katika mwaka uliopita ni pamoja na kudahili wanafunzi 90,712 katika vyuo vya VETA, miongoni mwao wakiwemo wa kike 31,033 na wenye mahitaji maalum 423; kufanya tafiti tisa (9) za soko la ajira katika maeneo ya Umeme, Uchapishaji, Upambaji, Uvuvi, Mitambo ya treni, Ujenzi, Biashara, Usafirishaji na Ufundi wa Magari.
Ameyataja mafanikio
mengine kuwa ni ujenzi vyuo vipya vya VETA, vikiwemo vyuo 25 vya wilaya
vilivyojengwa na VETA kwa kutumia nguvukazi ya ndani; uratibu wa ujenzi wa chuo
cha Mafunzo ya Ufundi Stadi na Huduma cha mkoa wa Kagera ambacho kilikuwa
kikijengwa kwa msaada wa Serikali ya China; uratibu na ufuatiliaji wa ujenzi na
upanuzi wa vyuo vingine ambavyo ni pamoja na Chuo cha VETA Karagwe, Nyasa,
Kongwa, Kasulu, Ruangwa, Nyamidaho, Njombe, Geita, Simiyu na Rukwa. Pia VETA
ilifanya upanuzi na ukarabati wa miundombinu ya Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi
Morogoro (MVTTC), Chuo cha Hoteli na Utalii cha VETA Arusha (VHTTI), Chuo cha
Ufundi Stadi Busokelo na Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Arusha.
Pia jumla ya wabunifu 277 kutoka vyuo vya ufundi stadi na mfumo usio rasmi
walitambuliwa kupitia Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu
(MAKISATU).
Katika ziara hiyo,
Katibu Mkuu katika aliambatana na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
Ndg. Moshi Kabengwe.
No comments:
Post a Comment