Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Prof. Adolf Mkenda, amewaasa na kuwakumbusha
watendaji wa Wizara hiyo na taasisi zake kuweka na kutekeleza mikakati
mbalimbali yenye kutafsiri kwa vitendo maono ya nchi kuhusu elimu ujuzi.
Prof. Mkenda ametoa
wito huo wakati wa kikao cha pamoja kati ya menejimenti na watendaji waandamizi
wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi Stadi (VETA), kilichofanyika kwenye Chuo cha VETA Dodoma, leo tarehe 17
Novemba 2022.
Kikao hicho kilikuwa
kikitathmini utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa vyuo 25 vya ufundi stadi vya
wilaya, awamu ya kwanza, sambamba na kujadili mkakati wa ujenzi wa vyuo vya
ufundi stadi kwenye wilaya 63 katika awamu ya pili.
Amewaasa kufanya kazi
kwa kuzingatia matokeo ili utekelezaji wa maono ya elimu ujuzi uonekane wazi.
"Nchi yote sasa
inazungumza kuhusu elimu ujuzi ambapo kiuhalisia ni ufundi stadi. Hivyo, sisi
tuna jukumu kubwa la kutafsiri na kuonesha matokeo zaidi," amesema.
Akizungumza kuhusu
mkakati wa ujenzi wa vyuo vipya 63 vya ufundi stadi vya wilaya, Prof. Mkenda
amewaagiza watendaji kufanya upembuzi wa kina juu ya namna bora ya kutekeleza,
ikiwemo kupima faida na changamoto za kutumia nguvukazi ya ndani (Force
Account); kutumia wakandarasi au kukabidhi taasisi zingine za Serikali.
Awali, wakati
akiwasilisha taarifa kwa Waziri, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA. Anthony
Kasore, alisema kuwa ujenzi wa vyuo 25 vya ufundi stadi vya wilaya uliokuwa
ukitekelezwa na VETA kwa kutumia Force Account uko katika hatua za mwisho na
unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba mwaka huu.
Sambamba na ujenzi,
VETA pia ilikuwa ikitengeneza samani za vyuo hivyo kupitia karakana zake ambapo
alisema kuwa utengenezaji wake umefikia asilimia 90 na kwamba karibu nusu ya
samani zimeshasambazwa kwenye vyuo vipya vya VETA.
Kuhusu ujenzi wa vyuo
63 vya awamu ya pili, CPA Kasore amewasilisha mapendekezo ya ujenzi ikiwemo
wilaya ambazo zimeleta maombi na kueleza kuwa baadhi zimeshatenga maeneo kwa
ajili ya ujenzi huo.
No comments:
Post a Comment