Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
imekipatia Chuo cha VETA Mikumi magari mawili kwa ajili ya kuimarisha utoaji mafunzo
kwa vitendo chuoni hapo.
Akizungumza wakati wa hafla ya Maadhimisho ya Miaka 25 na Mahafali ya Chuo cha VETA Mikumi
tarehe 25 Novemba 2022, Meneja
wa TRA Mkoa wa Morogoro, Ndugu Godwin Barongo, aliyekuwa mgeni rasmi kwenye
hafla hayo amesema Mamlaka hiyo imeguswa na changamoto ya uhaba wa magari ya
kufundishia chuoni hapo na kuamua kutoa magari hayo.
"Tumeguswa na changamoto ya ukosefu wa magari inayowakabili katika utoaji wa mafunzo...sisi hatuna magari mapya bali tutawapa magari mawili ambayo yameshatumika lakini yatawafaa sana katika kutoa mafunzo," amesema
Ndugu Barongo amewataka wahitimu
wa chuo hicho kutumia vyema ujuzi walioupata kwenye fani mbalimbali kuanzisha
shughuli zao na kujipatia kipato huku akiwasisitiza kujituma kwenye kazi, kuwa
waaminifu na kujali wateja.
Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Mashariki, Ndugu Wilhard Soko, ameishukuru TRA kwa kuipatia VETA magari hayo na kuiomba kuendelea kushirikiana na VETA kwenye nyanja mbalimbali ili kuendelea kuzalisha mafundi stadi mahiri.
Ndugu Soko amewasihi wazazi wanaoishi karibu na chuo hicho kukitumia vyema kwa kuwapeleka vijana wao kujipatia ujuzi utakaowasaidia kuendesha maisha yao.
Awali, Mkuu wa Chuo cha VETA Mikumi, Ndugu Marynurce Kazosi, amesema chuo chake kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa magari ya kufundishia kozi za udereva na ufundi wa magari na kumuomba mgeni rasmi kusaidia upatikanaji wa magari ili kutatua changamoto hiyo.
Amesema katika kuadhimisha miaka 25, chuo hicho kinajivunia mafanikio mbalimbali ikiwemo kutoa mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana ambao asilimia kubwa wameajirika pamoja na kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi kwa kutumia wataalamu wake.
Mahafali hayo yalihusisha jumla ya wahitimu 204 (wavulana 126 na wasichana 78) wa mafunzo ya ngazi ya pili na ya tatu chuoni hapo katika fani za Useremala, Uashi, Umeme wa Majumbani, Ufundi Mitambo, Ufundi Magari, Uandaaji Chakula, Huduma na Mauzo ya Vyakula na Vinywaji, Uongozaji Watalii pamoja na Mapokezi.
Chuo cha VETA Mikumi kilijengwa mwaka 1990 kwa ushirikiano
kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ireland na kutambulika kama chuo cha ufundi stadi cha
Wilaya ya Kilosa(KDVTC) na baadaye kukabidhiwa VETA mwaka 1997.
No comments:
Post a Comment