Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)
imeikabidhi Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mitaala 10 na mihutasari
minne ya ufundi kwa ajili ya shule za msingi zenye mikondo ya ufundi (Post
Primary Technical Centres-PPTC).
Mitaala hiyo imekabidhiwa kwa Kamishna wa Elimu
nchini Dkt. Lyabwene Mtahabwa na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA.
Steven Kwetukia, kwenye kikao cha Kamati ya Kitaifa ya utekelezaji wa mradi wa Elimu
Bora kwa Ukuaji wa Afrika Awamu ya Pili, (Better Education for Africa’s
Rise-Phase Two-BEAR II) kilichofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 10 Novemba,
2022.
Mradi wa BEAR II uliofadhaliwa na UNESCO na
Serikali ya Korea ulilenga kuongeza ubora na umuhimu wa Elimu ya Ufundi na
Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET) na kubadili mtazamo juu ya elimu hiyo ambapo
utekelezaji wake umefanyika kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2020 hadi
2022.
Mkurugenzi wa Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA, Ndugu
Abdallah Ngodu, ameainisha mitaala iliyotengenezwa na kukabidhiwa kuwa ni ya masomo
ya Uchumi wa Nyumbani, Kilimo cha Bustani, Useremala, Umeme wa Majumbani, Ufugaji,
Uchomeleaji Vyuma, Uashi, Ufundi Magari, Ufundi Bomba na Kazi za Mikono. Pia
VETA imeandaa mihtasari ya masomo ya Kiswahili, Kingereza, Hesabu na Uraia.
Ndugu Ngodu ametaja mafanikio yaliyopatikana
kupitia mradi huo kuwa ni pamoja na uandaaji wa Mitaala ya uchakataji wa
chakula na Upangaji na Upambaji wa Mazingira ya Ndani ya Nyumba (Interior
Design) kwa ngazi ya 4 hadi 6 za elimu ya ufundi, pamoja na uwezeshaji vifaa vya
kisasa vya mafunzo ya uchakataji wa vyakula kwa chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi
Morogoro (MVTTC). Kupitia mradi wa BEAR II watumishi wa MVTTC walipatiwa
mafunzo kuhusu masuala mbalimbali ya kiutendaji, utawala bora na mpango mkakati
pamoja na kuwezeshwa vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya kuimarisha mafunzo kwa Masafa
kidigitali kwenye chuo hicho.
Amesema shughuli nyingine zilizofanywa na VETA ni
kufundisha wakulima wa Halmashauri za Wilaya za Morogoro, Mvomero na Manispaa
ya Morogoro kuhusu mnyororo wa thamani katika zao la muhogo, Uaandaji
wa Sherehe na Upambaji.
No comments:
Post a Comment