Wananchi wilayani
Mbarali mkoa wa Mbeya wameanza kunufaika na mafunzo ya ufundi stadi katika chuo
kipya cha VETA wilayani humo, ambapo tayari wananchi 35 wamehitimu mafunzo ya
muda mfupi katika chuo hicho.
Hafla ya kukabidhi
vyeti wahitimu hao katika fani za Uashi
na Udereva imefanyika tarehe 19 Novemba 2022 ambapo Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Wilaya ya Mbarali, Ndugu Missana Kwangura amewatunuku vyeti.
Mafunzo hayo
yametolewa kupitia jitihada za Mkurugenzi huyo za kuhakikisha wananchi wa
Wilaya ya Mbarali wanapata stadi zinazohitajika Wilayani hapo katika
kufanikisha shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Wahitimu hao
walipatiwa mafunzo kwa mwezi mmoja kuanzia tarehe 21 Septemba hadi 21 Oktoba,
2022 ambapo wananchi 27 kati yao walifundishwa udereva na nane uashi.
Msimamizi wa chuo
hicho ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha VETA Mbeya, Mhandisi Hassan Kalima,
amesema kwenye fani ya uashi wananchi hao wamefundishwa kutengeneza tofali bora
za saruji kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya Serikali wilayani hapo.
Chuo cha Ufundi Stadi
cha Wilaya ya Mbarali ni miongoni mwa vyuo vipya 25 vilivyojengwa na VETA kwa
kutumia nguvukazi ya ndani (Force account). Chuo hicho kinatarajia kuanza kutoa
mafunzo ya muda mrefu mwezi Januari, 2023 katika fani za Ushonaji, Umeme wa
Majumbani pamoja na Uhazili na Kompyuta.
No comments:
Post a Comment