Mkuu wa Wilaya ya
Ngorongoro, Mhe. Raymond Mwangwala, ameitaka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi Stadi (VETA) kupitia chuo cha VETA cha Wilaya ya Ngorongoro kuanzisha
fani za kilimo, ufugaji, hoteli na utalii ili kuwezesha wananchi wa Ngorongoro
kupata stadi za kuboresha shughuli zao.
Akizungumza wakati wa
mahafali ya kwanza ya chuo cha VETA Ngorongoro mkoani Arusha tarehe 2 Desemba,
2022, Mhe. Mwangwala amesema shughuli kubwa wanazofanya wananchi wa Ngorongoro
ni za kilimo, ufugaji, hoteli na utalii hivyo wanahitaji mafunzo yatakayowapa
ujuzi wa kuendesha shughuli hizo kitaalamu.
“Pamoja na kozi za
ufugaji na kilimo, kozi zingine zinazohitajika wilayani hapa kuendana na
shughuli za kijamii zinazozunguka chuo hiki (VETA Ngorongoro) ni za Utalii,
hoteli na zile zinazohusiana na miundombinu ya maji,”amesema.
Aidha, Mhe. Mwangwala
amepiga marufuku sherehe za bukwa zinazohususisha wazazi kuwaozesha wanafunzi
na kuwataka wananchi wa Ngorongoro kuchangamkia fursa za mafunzo ya ufundi
stadi.
DC Mwangwala ameagiza
wadau mbalimbali kushirikiana na chuo hicho katika kuwezesha upatikanaji wa magari
ya kuendesha kozi za udereva.
Mkurugenzi wa VETA
Kanda ya Kaskazini, Bi. Monica Mbelle, aliwasihi wananchi kutumia fursa za
mafunzo zinazopatikana kwenye vyuo vya VETA kwenye kanda hiyo kujipatia ujuzi
utakaowasaidia katika kuendesha shughuli zao kwa ufanisi.
Bi. Mbelle alisema
chuo hicho kinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa magari ya kufundishia kozi
za udereva na kumuomba mgeni rasmi kusaidia upatikanaji wa magari ili kutatua
changamoto hiyo.
Mkuu wa Chuo cha VETA Ngorongoro, Ndugu Gabriel Sikoi, alisema chuo hicho kilipokelewa kutoka kwa wananchi kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro mwaka 2019 na VETA ilifanya ukarabati na ukamilishaji wa majengo hayo na kuanza kutoa mafunzo mwezi Januari, 2021
Awamu ya pili ya
ujenzi inahusisha ujenzi wa mabweni mawili, bwalo la chakula, madarasa mawili,
nyumba ya watumishi ya familia mbili ambapo ujenzi umefikia asilimia 81.
Ndugu Sikoi alitaja
baadhi ya changamoto zinazokabili chuo hicho kuwa ni mwamko mdogo wa jamii
inayozunguka chuo kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi na ukosefu wa magari ya
kuendeshea kozi za udereva.
Mahafali ya kwanza ya
Chuo cha VETA Ngorongoro imehusisha wahitimu 47 (wavulana 29 na wasichana 18)
katika fani za umeme wa majumbani, uashi na ushonaji. Wanafunzi wengine 89 (wavulana
53 na wasichana 36) wanaendelea na masomo chuoni hapo.
No comments:
Post a Comment