Mkuu wa Wilaya ya
Dodoma, Mhe. Jabir Shekimweri, ameishauri Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
Stadi (VETA) kushirikiana na taasisi za ujenzi nchini kuwezesha ujenzi wa
hosteli za wanafunzi ili kukabiliana na changamoto ya makazi kwa wanafunzi
iliyopo kwenye vyuo vingi vya VETA nchini.
Akizungumza wakati wa
mahafali ya 39 ya Chuo cha VETA Dodoma leo tarehe 3 Desemba, 2022, Mhe.
Shekimweri amesema kuwa ujenzi wa hosteli za kutosheleza mahitaji ya wanafunzi
utawezesha wanafunzi wa ufundi stadi kupata mafunzo yao kwa ufanisi zaidi.
“NI wakati sasa VETA
ifikirie kufanya makubaliano ya mashirikiano na Taasisi za ujenzi kama TBA na
NHC ili Taasisi hizi zijenge hosteli za kutosheleza mahitaji ya wanafunzi na
kuziendesha kwa muda fulani na baadaye zikabidhiwe VETA,”amesema
Uhaba wa hosteli
zinazotosheleza idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kwenye vyuo vya VETA ni
miongoni mwa changamoto zilizowasilishwa na wahitimu wa mafunzo ya ufundi stadi
kwenye hotuba yao waliyoisoma kwa Mgeni Rasmi wa mahafali hayo Mhe. Shekimweri.
Aidha, Mhe Shekimweri
ameahidi kuratibu vikundi vya wahitimu wa fani mbalimbali chuoni hapo kupata
mikopo ya asilimia 10 inayotengwa na Halmashauri ili waweze kujiajiri.
Mkurugenzi wa Utahini
na Utunuku wa VETA, Ndugu Francis Komba, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa
VETA kwenye mahafali hayo, amesema VETA imeendelea kuhakikisha ubora wa mafunzo
yanayotolewa kwenye vyuo vyake ili kuzalisha nguvu kazi mahiri yenye ujuzi
unaohitajika kwenye soko la ajira.
Awali Mkuu wa Chuo
cha VETA Dodoma, Ndugu Stanslaus Ntibara, amesema chuo chake kinashirikiana na
wadau wa ndani na nje ya nchi katika kutoa mafunzo ya ufundi stadi kwa makundi
mbalimbali na kuyawezesha makundi hayo kushiriki kikamilifu kwenye shughuli
mbalimbali za uchumi.
“Baadhi ya wadau
tulioshirikiana nao katika mwaka wa masomo unaokwisha ni pamoja na Ofisi ya
Waziri Mkuu (Ufadhili wa Wanagenzi 586), Wizara ya Kilimo (Wanagenzi 60),
Taasisi ya Elimu Tanzania (TEA) Wanagenzi (407), Shirika la Maendeleo la
Ujerumani (GIZ) na Shirika la Maendeleo la KOREA Kusini (KOICA) chini ya mpango
wa E4D (Wanafadhili wanafunzi 2,200),”amesema
Mahafali hayo
yamehusisha jumla ya wahitimu 493 wa mafunzo ya ufundi stadi kati yao 258
wamehitimu katika fani za muda mrefu hatua ya pili (level II) na ya tatu (level
III) na 235 wamehitimu mafunzo ya uwanagenzi yaliyotolewa kwa muda wa miezi
sita kupitia ufadhili wa ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana,Ajira na Wenye
Ulemavu.
Wahitimu hao wamesoma
fani za Useremala,Upishi,Ufundi Bomba, Uungaji na Uchomeleaji Vyuma, Umeme wa
Majumbani, Ukarabati na Ujenzi wa Barabara, Uchinjaji na Uchakataji wa Nyama,
Upakaji Rangi na Uandishi wa Alama, Elektroniki,Ukerezaji wa Vyuma, Uashi,
Huduma ya Mapokezi, Ufundi Magari pamoja na Uhudumu na Uuzaji wa Vyakula na
Vinywaji.
No comments:
Post a Comment