CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Friday 2 December 2022

Prof. Mkenda: Mageuzi ya Elimu nchini kuhakikisha Elimu Ujuzi inapatikana

 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema mageuzi ya elimu yanayokuja yanakwenda sambamba na kuandaa mazingira ya kuhakikisha elimu ujuzi inapatikana.

Mhe. Mkenda ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa kikao cha pamoja cha  Menejimenti ya Wizara na ile ya VETA chenye lengo la kujadili kwa pamoja rasimu ya  mkakati wa utekelezaji wa ujenzi wa VETA 63 za wilaya na moja ya mkoa.

Amesema moja ya eneo linaloangaliwa katika kutoa elimu ujuzi ni kupitia vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) hivyo ni   vizuri kuwa na mikakati thabiti ya kuhakikisha VETA 63 za Wilaya na moja ya mkoa ujenzi unaanza.

 "Nataka twende pamoja, katika kuweka historia hii; tunakwenda kufanya mageuzi makubwa ya elimu kwa kuhakikisha  tunatoa elimu ujuzi, sasa kazi ya mapitio ya Sera  na Mitaala inakwenda vizuri na tuko tayari kufanya wasilisho kwa ajili ya mjadala wa Kitaifa, sasa nataka huku kwenye ujenzi wa VETA 63 ambako elimu ujuzi inapatikana kuende kwa kasi na kwa  wakati ,"amesema Prof. Mkenda

Amesema katika mwaka wa fedha 2022/23 Wizara imetenga fedha Bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa VETA hizo hivyo  kutaka   mkakati wa kuhakikisha ujenzi unaanza mapema na kujengwa kwa usahihi kwa kuzingatia taratibu zote husika.                                                                                                                  

Akizungumzia maandalizi ya ujenzi wa VETA hizo Mkurugenzi wa Soko la Ajira, Mipango na Maendeleo wa VETA Mhandisi George Sambali, amesema mpaka sasa kati ya wilaya 63 zinazotarajiwa kujengewa vyuo vya VETA wilaya 59 tayari zimeshatenga maeneo yatakayo jengwa vyuo vya VETA.



No comments:

Post a Comment