Mamlaka ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa kushirikiana na Makampuni ya Mradi wa Ujenzi
wa Bomba la Mafuta Ghafi – East Africa Crude Oil Pipeline (EACOP) wanatarajia
kutoa mafunzo kwa vijana 170 nchini wanaoshiriki kwenye mradi huo.
Akizungumza wakati wa
uzinduzi wa mafunzo hayo tarehe 15 Februari, 2023 katika chuo cha VETA Tanga,
Kamishna wa Mafuta na Gesi kutoka Wizara ya Nishati, Ndugu Michael Mjinja
amesema mafunzo hayo yatatolewa kwa wafanyakazi 170 wanaotekeleza shughuli
mbalimbali kwenye mradi wa bomba la mafuta ambao wataboreshewa ujuzi wao ili
kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa mradi.
Ndugu Mjinja amesema
mafunzo hayo yanatolewa na kampuni ya Daqing Oilfield Construction Group Co.Ltd
(DOCG) kupitia kampuni ya Kimataifa ya Sunmaker Development and Consulting (TZ)
Ltd ambapo wahitimu wa mafunzo hayo watapatiwa vyeti vinavyotambulika kimataifa
vitakavyowawezesha kufanya kazi popote duniani.
Amesema washiriki wa
mafunzo hayo watapata utaalamu wa ufundi kwenye miradi inayohusiana na sekta ya
mafuta na gesi na kuweza kutumia utaalamu huo kwenye mradi wa bomba la mafuta
na miradi mingine nchini ili kukuza maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi nchini
Tanzania.
Walimu wa fani
mbalimbali katika chuo cha VETA cha Mkoa wa Tanga wanatarajia kunufaika na
mafunzo hayo yatakayotolewa chuoni hapo.
Miongoni mwa utaalamu
utakaotolewa kupitia mafunzo hayo ni wa ukaguzi wa afya, usalama na mazingira,
uendeshaji wa mashine ardhini, uendeshaji wa mitambo pamoja na ufundi wa umeme
na vifaa mbalimbali.
Mwanasheria wa VETA,
Wakili Dora Mweta aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa VETA kwenye hafla hiyo
amesema kuwa VETA inasikia fahari kushiriki kwenye mradi huo wenye manufaa makubwa kwa Taifa ambao pia unatoa fursa
nyingi za ajira kwa vijana.
Amesema mafunzo
yakayotolewa katika chuo cha VETA Tanga ambayo walimu wa VETA watashiriki,
yatawaongezea ujuzi walimu hao na kuwapa uzoefu kwenye eneo la mafuta na gesi
na hatimaye walimu hao kuwafundisha wanafunzi katika chuo hicho.
Wakili Mweta alitoa
rai kwa makampuni na wadau mbalimbali kuiunga mkono Serikali katika kuwasomesha
vijana na kuwawezesha kupata ajira.
Uzinduzi wa mafunzo
hayo umehusisha Wizara ya Nishati, Serikali ya Mkoa wa Tanga na watendaji wa
mashirika ya TPDC, EWURA, VETA na Chuo cha Ufundi Arusha ambapo washiriki wa
hafla hiyo walipata fursa ya kutembelea
eneo lilipowekwa jiwe la msingi
la mradi huo na maeneo yatakapowekwa matanki ya mafuta.
Ujenzi wa mradi wa
bomba la mafuta ghafi la kutoka Hoima - Magharibi mwa Uganda mpaka kwenye
bandari ya bahari ya Hindi, Tanga wenye urefu wa jumla ya Kilometa 1,443
zikiwemo 1,115 zitakazojengwa ndani ya ardhi ya Tanzania unatarajia kuzalisha
ajira zipatazo 10,000.
No comments:
Post a Comment