Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali (PAC) ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wake Mhe. Japhet
Hasunga imeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa mabweni ya Chuo cha
VETA cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC).
Akizungumza wakati wa
ziara ya kukagua mradi huo leo tarehe 19 Machi, 2023, Mhe Hasunga amesema
kamati yake imefanya ziara kwenye mradi huo ili kujiridhisha endapo fedha
zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya ujenzi wa mabweni hayo zimetumika kama
ilivyokusudiwa.
“Baada ya kupata
taarifa ya CAG pamoja na taarifa ya mradi kutoka kwa Katibu Mkuu, tumeyaona
majengo ya mabweni na yako kwenye hali nzuri yanapendeza na yamekamilika kwa
asilimia karibu 100,”amesema
Aidha,kamati hiyo
imeiagiza Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha
samani kwa ajili ya mabweni hayo zinapatikana haraka ili mabweni hayo yaanze
kutumika kama ilivyokusudiwa.
Kamati hiyo pia
imeaigiza Wizara hiyo kuhakikisha samani za chuo hicho na nyingine zinazotumika
kwenye vyuo vya VETA nchini zinatengenezwa na VETA kwa kuwa Mamlaka hiyo ina
wataalamu wa kutosha kwenye vyuo vyake wenye ujuzi wa kutosha kufanya kazi
hiyo.
Naibu Waziri wa
Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga amesema Wizara yake itafanyia
kazi maelekezo ya Kamati hiyo na kuhakikisha fedha kwa ajili ya kutengeneza
samani za mabweni hayo takribani shilingi milioni 54 zinapatikana kabla ya
kumalizika kwa mwezi Machi, 2023 ili VETA iweze kutengeneza samani hizo.
Naye Katibu Mkuu wa
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, amesema mradi
huo umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.07 na kuahidi kuwa Wizara yake
itahakikisha mabweni hayo yanatunzwa Ili yanufaishe watanzania wengi.
Awali akiwasilisha
taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa kamati ya Bunge kwa niaba ya Katibu
Mkuu, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema kukamilika kwa
mabweni hayo kutaongeza udahili katika chuo hicho kwa nafasi za bweni kutoka
walimu tarajali 120 hadi 216.
Amesema mpango wa
VETA ni kuongeza udahili wa walimu tarajali kufikia wanafunzi 660 kwa mwaka
ifikapo mwaka 2025/26 ambapo wanafunzi 320 watapata mafunzo ndani ya chuo
(incampus) na 340 ni wanafunzi
watakaopata mafunzo kwa njia ya masafa.
No comments:
Post a Comment