Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Kasore, amewakumbusha Maafisa Ununuzi na Ugavi wa Mamlaka hiyo kufanya kazi kwa weledi na uadilifu ili kufanikisha utekelezaji wa shughuli za Mamlaka hiyo.
CPA Kasore ametoa
wito huo tarehe 11 Machi, 2023 wakati wa kikao kazi kati ya Menejimenti ya
VETA Makao Makuu na Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi wa Kanda na vyuo vya VETA
nchini kilicholenga kujadili utekelezaji wa shughuli za kada hiyo na kuweka
mikakati ya kuboresha utendaji kazi.
CPA Kasore amesema
wataalamu wa ununuzi na ugavi wana mchango mkubwa katika kufanikisha malengo ya
VETA na kwamba ni muhimu wakatekeleza
kazi zao kwa kuzingatia misingi na taratibu za taaluma yao na taratibu za
utumishi wa umma.
“Napenda kuwakumbusha
umuhimu mlionao katika kufanikisha shughuli za Mamlaka ambazo ni za kutoa
mafunzo ya ufundi stadi kwa watanzania…Nawasihi sana mtekeleze majukumu yenu
kwa ufanisi ili kutokwamisha shughuli za Mamlaka na hatimaye kufanikisha malengo
tuliyojiwekea,” amesema
Aidha, CPA Kasore
amewaasa Maafisa hao kutoa ushauri wa kitaalamu mara kwa mara ili kuwasaidia
viongozi kwenye maeneo yao kufanya maamuzi sahihi na kuwezesha ufanisi katika
utekelezaji wa shughuli za Taasisi hiyo.
Awali, Kaimu Mkuu wa
Kitengo cha Ununuzi na Ugavi wa VETA, Bi. Witness Mgimba, amesema utendaji kazi
bora wa maafisa ununuzi na ugavi utasaidia kuongeza tija kwenye Mamlaka hiyo na
kuwataka Maafisa hao kuzingatia ufanisi, uadilifu na weledi.
Bi. Mgimba amewasihi
maafisa ununuzi kujiongeza kwenye kazi zao kwa kujifunza masuala mbalimbali
kuendana na mabadiliko yanayotokea kwenye taaluma hiyo na kuwataka kuwa na
utayari wa kupokea mawazo na ushauri wenye lengo la kuleta ufanisi katika
shughuli mbalimbali.
Kikao kazi hicho kimehudhuriwa na Maafisa Ununuzi na Ugavi 45 kutoka ofisi za kanda na vyuo vya VETA pamoja na watendaji waandamizi wa Mamlaka hiyo.
No comments:
Post a Comment