Wanawake katika
kijiji cha Mlowa Bwawani, Wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma wamejitokeza kwa
wingi kuchangamkia fursa ya maandalizi ya kuanza kwa mradi wa ujenzi wa Chuo
cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma, ujenzi ambao kwa sasa
upo katika hatua za awali za kupanga majengo na uchimbaji wa msingi.
Ujenzi wa Chuo cha
Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chamwino ni sehemu ya mradi mkubwa wa ujenzi wa vyuo
64 vya ufundi stadi vya wilaya na kimoja cha Mkoa wa Songwe unaotekelezwa na
serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Akizungumza leo,
tarehe 5 Aprili 2023, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi
wa chuo hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Dkt.
Franklin Rwezimula, amewapongeza wananchi wa kijiji hicho, hasa wanawake kwa
kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa za maandalizi ya awali ya Ujenzi wa
chuo.
Amesema, tofauti na
maeneo mengine ambapo wanaume wanakuwa wengi, katika eneo hilo, wanawake
wamekuwa wengi kuliko wanaume.
Rwezimula ametoa wito
kwa wanaume kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa za ujenzi wa chuo hicho
kama walivyofanya wanawake.
“Wananchi pia wanashiriki kwa wingi katika ujenzi wa hiki chuo katika kutoa nguvu kazi, nihamasishe wananchi wa kata hii wajitokeze kwa wingi waje wafanye kazi, Kazi hizi sio za bure zinalipwa, malipo watakayopata katika kazi hizi zitawasaidia kuinua uchumi wa kaya zao pamoja na uchumi wa kata,” amesema.
“Nimefurahi kuona washiriki wengi ni akina
mama kama mnavyojua akina mama ndio wanatunza familia wanachokipata kinaenda
kutunza watoto lakini nihamasishe akina baba pia wasibaki nyuma mje mshiriki,
mama akikusanya na wewe ukakusanya mkachanganya kinakuwa kikubwa”.
Kwa mujibi wa Dkt.
Rwezimula, chuo hicho kitatoa kozi ambazo zitawezesha vijana wa Chamwino
kujipatia ujuzi kwenye fani mbalimbali na kuweza kushiriki katika shughuli za
kiuchumi.
Dkt. Rwezimula
alimshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa pesa ambazo zitajenga
vyuo vya VETA 64 nchi nzima.
Diwani wa Kata ya
Mlowa ndugu Andrew Mseya amemhakikishia Dkt. Rwezimula ushiriki wa wananchi
wake kwenye ujenzi huo na usalama wa vifaa vya ujenzi vitakavyoletwa kwa ajili
ya ujenzi.
Mkuu wa kitengo cha
Sheria VETA, Bi.Dora Mweta akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa VETA, ametoa wito
kwa wananchi wa Mlowa Bwawani kuona ujio wa chuo hicho kuwa ni kwa manufaa yao
na kwa sababu ya kuthaminiwa na Serikali, hivyo wajitokeze kwa wingi kujitolea
katika Ujenzi.
Ameongeza kuwa ujenzi
wa chuo hicho utaongeza ukuaji wa eneo hilo, kwani kutavutia maendeleo ya mji
huo, kutaleta mabadiliko mengi kutaleta ikiwemo umeme, maji na huduma zingine
za kijamii.
No comments:
Post a Comment