Naibu Katibu Mkuu, Wizara
ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Franklin Rwezimula, jana, tarehe 4 Mei
2023 alifanya ziara katika Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)
na kuelekeza mambo kadhaa yanayoweza kuchangia katika kuongeza ubora wa
mafunzo, hivyo umahiri wa wanafunzi wa ufundi stadi.
Akizungumza na Menejimenti
ya VETA Makao Makuu, miongoni mwa mambo aliyoelekeza Dkt, Rwezimula ni
kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya vyuo vya ufundi stadi na viwanda ambako
vijana wanaweza kupata mafunzo mengi ya vitendo na kujifunza teknolojia za
kisasa zaidi, sambamba na kuboresha karakana kwa kununua vifaa vya kisasa na
kuona namna ya kutumia wabobevu wa ufundi kutoka mfumo usio rasmi kusaidia
kwenye mafunzo ya vitendo.
Mambo mengine aliyoyaagiza,
Dkt. Rwezimula ni pamoja na kufanya marejeo ya mara kwa mara ya mitaala ili kwenda
sambamba na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko la ajira ili utoaji
mafunzo uendane na mahitaji ya soko la ajira na shughuli za kiuchumi katika
jamii mbalimbali na pamoja na kufanya ufuatiliaji wa wahitimu ili kutambua
wanavyokubalika na wanavyofanya kazi kwenye soko la ajira.
“Tunapokwenda kwenye
mabadiliko ya mitaala ya elimu nchini, ufundi stadi ni suala la msingi. Pia
uchumi wa sasa uko kwenye ufundi zaidi. Kwa hiyo, ni muhimu kutambua na
kuzingatia majukumu ya VETA katika kusaidia mwelekeo huu,” alisema.
Kwa upande mwingine, Dkt.
Rwezimula ameishauri VETA kushirikiana na wadau ili kusaidia wahitimu wa ufundi
stadi kupata mikopo na misaada mingine ya kifedha ili kuwasaidia kujiajiri.
Awali, Mkurugenzi Msaidizi
wa Idara ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia, Dkt. Ethel Kasembe, alieleza juhudi za Wizara katika
kusaidia uboreshaji mafunzo kuwa ni pamoja na kuandaa maandiko ya kuomba fedha
za kununua vifaa vya karakana kwa ajili ya mafunzo kwenye vyuo vya VETA nchini.
Akitoa taarifa ya maendeleo
ya uendeshaji wa shughuli za VETA, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony
Kasore, licha ya kutaja mafanikio mbalimbali alitaja uhaba wa vifaa kwenye
karakana za mafunzo, uhaba wa watumishi na ukomo mdogo wa bajeti ikilinganishwa
na hali ya kukua na kupanuka kwa Mamlaka kuwa ni miongoni mwa changamoto.
Alitaja miongoni mwa
mafanikio kuwa ni pamoja na kufanya tafiti kumi (10) za soko la ajira; kutoa
mafunzo kwa wajasiliamali 708 kupitia programu ya INTEP katikamwaka 2022/2023;
kuibua wabunifu 82 kutoka vyuo vya ufundi stadi na 573 kutoka mfumo usio rasmi
walitambuliwa kupitia Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu
(MAKISATU) katika kipindi cha mwaka 2019-2022 na kuboresha na kufanya marejeo
ya mitaala 48 kati ya 89 ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi katika mwaka wa
fedha 2022/2023 na umaliziaji wa vyuo 25 vya
wilaya, pamoja na utengenezaji wa samani zake.
CPA Kasore alitaja
mafanikio mengine kuwa ni kudahili wanafunzi 46,379 kwenye vyuo vya VETA katika
kipindi cha nusu mwaka 2022/2023 na wanafunzi 243 wenye mahitaji maalum
Hata hivyo, CPA Kasore alitaja changamoto zinazoikabili Mamlaka kuwa ni
pamoja na ukomo
wa bajeti kutotosheleza mahitaji ya shughuli za Mamlaka kwa ujumla; mahitaji ya
vifaa na upungufu wa watumishi.
“Mathalani, mwaka 2022/2023 Mamlaka imetengewa bajeti
ya Shilingi 54,000,000,000/= ikilinganishwa na mahitaji halisi ya Shilingi 99,600,000,000/=.
Mahitaji ya vifaa vyuo vyote vya VETA ikiwemo 65 vinavyojengwa yanakadiriwa
kufikia TZS. 211,047,890,669.00. Pia tuna upungufu wa watumishi 1282,”
alifafanua.
Alimuomba Naibu Katibu Mkuu kwa niaba ya Wizara
kupokea maombi ya kuongezewa bajeti ya uendeshaji kutokana na kukua kwa Taasisi
hususani kuongezeka kwa idadi ya vyuo ambapo kufikia 2024 VETA itakuwa na vyuo
zaidi ya 140 ikilinganishwa na vyuo 51 vilivyopo sasa. Vilevile gharama za
uendeshaji mafunzo zimekuwa zikipanda mwaka hadi mwaka.
Vilevile kusaidia
upatikanaji wa vibali vya ajira kwa ajili ya watumishi walimu na wasio walimu
ili kufanikisha kuanza kwa mafunzo katika vyuo vipya vinavyokamilika kujengwa
na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya vifaa vya mafunzo (tools and equipment)
kwa ajili ya vyuo vya zamani na vyuo vipya 33 ambavyo ujenzi unakamilishwa.
No comments:
Post a Comment