Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, tarehe 17 Mei
2023 amefungua rasmi Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Ngorongoro na
kuziagiza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) na Wakala wa
Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuhakikisha wanaboresha
miundombinu ya barabara na huduma za maji ya uhakika kwa ajili ya chuo hicho.
Akizungumza baada ya
kufungua chuo hicho, kilichopo katika eneo la Samunge, wilayani Ngorongoro,
Dkt. Mpango ameagiza TARURA kuweka mpango wa kujenga kwa kiwango cha lami
barabara inayoelekea chuoni hapo kutoka makutano ya barabara ya Mto wa Mbu
kwenda Waso (Ngorongoro) ili kurahisisha usafiri wa wananchi kwenda chuoni.
Vilevile, Dkt. Mpango
ameagiza RUWASA kuhakikisha inatafuta suluhisho la kudumu la changamoto ya
upatikanaji wa maji chuoni hapo ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira
bora yenye huduma za uhakika wa maji.
Dkt. Mpango
amewapongeza wananchi wa Kijiji cha Samunge, hususani kundi-rika la Erumeshari
kwa kuwa mstari wa mbele katika kuchangia shughuli za maendeleo baada ya
kuarifiwa kuwa kundi-rika la Erumeshari ndilo lililoanzisha ujenzi wa Chuo cha
Ufundi Stadi cha Wilaya ya Ngorongoro.
“Utaratibu huu wa kirika ni wa kuigwa. Utaratibu huu ni mzuri sana, popote nitakakopita nitawaambia waje kujifunza utaratibu huu wa kirika,” amesema.
Hata hivyo, Dkt. Mpango aliwaomba wananchi kuwahamasisha vijana wa jinsi zote kujiunga na fani mbalimbali za ufundi stadi Amesema Taifa sasa linaandaa mpango wa kuona kuwa wale wote wanaomaliza shule na masomo katika ngazi mbalimbali wanapata ujuzi utakaowawezesha kujiletea maendeleo.
Akitoa taarifa kuhusu
Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Ngorongoro, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Kasore, amesema
wazo la ujenzi wa chuo hicho lilianza mwaka 2010 kupitia kundi-rika la
Erumeshari katika jamii ya Wasonjo, wakati linamaliza muda wake (kutoka rika la
ujana kwenda uzee).
Amesema, kundi hilo
lilitaka kuacha alama ya kudumu katika jamii, hivyo wakaamua kujenga Chuo cha
Ufundi Stadi, hivyo wakaamua kukusanya michango ya fedha na mali zingine kwa
ajili ya kugharamia fidia ya eneo lenye ukubwa wa ekari 40.
Amesema, mwaka 2016, kundi-rika hilo lilianza ujenzi kwa kutumia nguvukazi zao na kufanikiwa kujenga majengo manne hadi hatua ya boma.
“Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha waliunga mkono juhudi hizo za wananchi na kushirikisha Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kukipokea na kuendeleza ujenzi wa Chuo hiki ili kuwa Chuo cha VETA cha Wilaya ya Ngorongoro. Mwaka 2019, Chuo hiki kilipokelewa na kuwekwa kwenye mpango wa Serikali wa uanzishaji wa vyuo vya ufundi stadi vya wilaya,”Amesema.
CPA Kasore amesema,
tangu kupokea chuo hicho, Serikali imekuwa ikitenga fedha kila mwaka na hadi
mwaka huu wa 2023, jumla ya Shilingi 1,793,911,814 huku uendelezaji ukifanyika
kwa awamu.
Amesema, chuo hicho kimeshaanza kutoa mafunzo, ambapo mwaka 2023 kimedahili wanafunzi 147 katika fani za Umeme, Uashi na Ushonaji, Teknolojia ya Nguo na Ubunifu wa Mitindo ya Mavazi.
Aidha, kwa
kushirikiana na wadau, chuo kimefanikiwa kuendesha mafunzo ya muda mfupi katika
fani za Usindikaji Maziwa; Uchakataji wa Ngozi; na Ufugaji Bora wa Nyuki ambapo
jumla ya wananchi 442 wamenufaika na mafunzo hayo.
No comments:
Post a Comment