CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Thursday 11 May 2023

Vijana 1000 kunufaika na mafunzo ya ufundi zana za kilimo kupitia ushirikiano wa VETA na AGRICOM

Vijana elfu moja (1000) nchini wanatarajiwa kunufaika na mafunzo ya Ufundi wa Zana za Kilimo, kupitia ushirikiano kati ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Kampuni ya Agricom. 

Hayo yamebainishwa tarehe 10 Mei, 2023, baada ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Agricom kuweka saini za  makubaliano ya ushirikiano wa kutoa mafunzo ya Ufundi wa Zana za Kilimo.


Kupitia ushirikiano huo, Kampuni ya Agricom ambayo inajishughulisha na kilimo na uuzaji wa vipuri na zana za kilimo,  itawezesha kuboresha utoaji mafunzo ya ufundi wa Zana za Kilimo kwa walimu na wanafunzi fursa ya kujifunza kwa vitendo zaidi na kupata uzoefu kwenye mazingira halisi ya kazi.

Akizungumza baada ya kuweka saini ya makubaliano ya ushirikiano, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, alisema VETA itashirikiana na Agrico

kutoa  mafunzo kwa mfumo wa Uanagenzi Pacha na kuandaa wakufunzi wabobezi (Master Trainers) ambao watatumika kuboresha umahiri wa wanafunzi kwenye fani za uungaji vyuma, ufundi magari pamoja na ufundi wa mitambo na zana za kilimo na hatimaye kuzalisha wahitimu wanaoendana na mahitaji ya soko la ajira.

CPA Kasore alivitaja vyuo vya VETA vitakavyohusika na utoaji mafunzo kwenye mradi huo kuwa ni Dakawa, Kihonda, Arusha (Oljoro), Manyara na Mpanda.

CPA Kasore alisema VETA itaendelea kuboresha utoaji mafunzo kwenye sekta ya kilimo ikiwa ni jitihada za kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita za kuwezesha vijana kushiriki kwenye kilimo.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Agricom Ndg. Alex Duffar, alisema ushirikiano huo utawezesha upatikanaji wa mafundi mahiri, wenye uzoefu watakaoweza kufanya ukarabati wa  zana  mbalimbali za kilimo na kuanzisha biashara zao.

Alisema vijana watakaohitimu mafunzo wataweza kufanya matengenezo kwenye vifaa na mitambo mbalimbali ya kilimo ikiwemo Matrekta, ‘Powertillers’, ‘Combine Harvesters’, mashine za kukaushia mazao na zana nyingine za kilimo.




No comments:

Post a Comment