Waratibu na Wasajili
wa vyuo vya VETA wamekutana jijini Dodoma kwa lengo la kujengewa uwezo katika
kuboresha usimamizi na uendeshaji wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi.
Kikao kazi hicho kinachofanyika kwa siku mbili katika Chuo cha VETA Dodoma, kimefunguliwa rasmi leo tarehe 7 Juni, 2023 na Kaimu Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi wa VETA, Ndg. Abdallah Ngodu akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa VETA.
Ndg. Ngodu amewataka
waratibu na wasajili hao kufuatilia kwa makini mada mbalimbali zilizoandaliwa
na kutoa maoni yao na hatimaye kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha utoaji wa
elimu na mafunzo ya ufundi stadi.
Mwakilishi wa Waratibu wa Mafunzo kutoka VETA Kanda ya Magharibi, Ndg. Charles Mpambwe, ameshukuru Uongozi wa VETA kwa kuandaa kikao kazi hicho ambacho amesema kitatumika kama sehemu muhimu ya kupeana mrejesho wa utekelezaji wa shughuli za utoaji mafunzo kwenye vyuo vya VETA na kubadilishana uzoefu ili hatimaye kuleta ufanisi katika mafunzo.
Miongoni mwa mada
zinazowasilishwa kwenye kikao kazi hicho ni upangiliaji wa karakana na
mazingira (Kaizen model), taarifa ya Mitaala iliyohuishwa, taarifa ya
ufuatiliaji na tathmini ya mafunzo, miongozo ya ufundishaji wa elimu jumuishi
kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum na taarifa ya utoaji mafunzo ya uanagenzi.
No comments:
Post a Comment