Mamlaka
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ikishirikiana na Shirika la
Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani (GIZ) kupitia programu ya Kukuza Ajira na
Ujuzi kwa Maendeleo Afrika (E4D), wameandaa Kongamano la Ujuzi na Ajira (Job
and Skills Fair) lenye kauli mbiu isemayo “Ufundi Stadi kwa Fursa zaidi za
Ajira” linalotarajiwa kufanyika katika viwanja vya Nyerere Square, tarehe 24
Agosti, 2023, jijini Dodoma.
Akizungumza
na waandishi wa habari,katika ofisi za VETA Makao Makuu jijini Dodoma leo
tarehe 22 Agosti,2023, Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi -VETA,
Ndg. Abdallah Ngodu aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa VETA amesema kongamano
hilo limelenga kuwajengea wananchi uelewa juu ya fursa za Ufundi Stadi
zitolewazo kupitia mradi wa E4D,kukuza uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa kwa
wanufaika wa kozi zilizotolewa katika vyuo vya VETA nchini chini ya mradi huo.
Ameongeza
kuwa wanufaika wa mradi huo watakutanishwa na Waajiri ili kushirikishana
taarifa za soko la Ajira kwa ambapo hadi sasa jumla ya Makampuni na viwanda 20
vimethibitisha kushiriki kwa kuonesha bidhaa na huduma zao lakini pia watapata
fursa ya kuthibitisha uhalisia wa umahiri na ujuzi wa wahitimu wa Mafunzo ya
Ufundi Stadi yatolewayo na VETA.
“Kongamano hili litawapa fursa wananchi ya
kujionee shughuli zifanywazo na wahitimu/wanufaika wa mradi wa E4DT pamoja na
kupata taarifa juu ya fursa za Mafunzo ya Ufundi Stadi zitolewazo katika vyuo
vya VETA nchini” amesema.
Amesema
hadi sasa jumla ya vijana 3,258 wamenufaika na mafunzo katika fani za Ufundi
Bomba wa majumbani, Ufundi Bomba
Viwandani na Ufundi wa Uchomeleaji Vyuma Viwandani (Industrial Welding) katika
vyuo vya VETA vya Dodoma, Manyara. Lindi na Manyara.
Kwa upande wake, Mshauri wa Programu wa Shirika la GOPA aliyewakilisha washirika wa Mradi, Bi Leah Dotto. amesema utekelezaji wa programu hiyo umekuwa na mafanikio kwa kuwa umewezesha vijana kujipatia ujuzi na baadhi yao wameweza kuajiriwa na wengine kujiajiri
Tanzania ni miongoni mwa nchi sita za
Afrika zinazotekeleza mradi wa Stadi za Ajira kwa Maendeleo Afrika (E4D)
unaofadhiliwa na Wizara ya Shirikisho la Ujerumani la Ushirikiano wa Kiuchumi
na Maendeleo (BMZ) na Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo la Korea (KOICA).
Mradi huo ulianza kutekelezwa mwezi Mei, 2022, ukilenga kutoa mafunzo ya muda
mfupi kwa vijana 4000 nchini ili kuandaa nguvu kazi itakayotumika katika kukuza
ajira kwenye miradi ya kimkakati inayotekelezwa hapa nchini.
No comments:
Post a Comment