Vijana 221 kutoka katika mazingira magumu wamehitimu mafunzo maalum ya ufundi stadi katika Chuo cha VETA cha Wilaya ya Kishapu kupitia ufadhili wa shirika lisilo la kiserikari la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Africa (WiLDAF) kwa kushirikiana na Shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), pamoja na serikali ya Finland.
WiLDAF imewezesha
vijana wa kike waliofanyiwa ukatili, kupewa mimba za utotoni na wenye ulemavu
kupata mafunzo hayo kupitia mradi wake wa “Chaguo Langu Haki Yangu”
Akizungumza wakati wa
kufunga mafunzo hayo, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Kaimu Mkurugenzi wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Abdallah Ngodu, lengo la ujenzi wa vyuo vya
VETA ikiwemo chuo cha VETA cha Wilaya ya Kishapu ni kupanua fursa za
upatikanaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchi nzima na kwa makundi
mbalimbali, ili kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi wa kutosha kulingana na
mazingira yaliyopo.
Amewaasa wahitimu hao
kutumia fursa hiyo kuleta maendeleo katika jamii na kuwa mabalozi kwa mabinti
wengine huko katika jamii.
“VETA tumeamua kusogeza huduma karibu na
wananchi ili wananchi wengi waweze kujiunga na kupata mafunzo haya ya ufundi
stadi na tunaamini kwa hapa Kishapu mmeona umuhimu wa uwepo wa chuo hiki, hivyo
tunaomba muendelee kushirikiana na chuo hiki kwa kuwaeleza wananchi umuhimu wa
mafunzo yanayotolewa,” ameongeza Ngodu
Kwa upande wake Mkuu
wa Chuo cha VETA Shinyanga, Magu Mabelele, ambaye ni msimamizi wa Chuo hicho
amesema kati ya vijana 221 waliodahiliwa, 101 walijiunga na Ushonaji; 39 Urembo
na Mapambo; 20 Uhazili na TEHAMA, 1Uchomeleaji na Uungaji Vyuma, 7 Udereva wa Magari,
22 Ufundi Umeme, 3 Ufundi Magari, 11 Ufundi Bomba, 12 Upishi na Uandaaji
Chakula na 5 Kudarizi.
Amesema, licha ya
kusaidia kuwapatia ujuzi vijana hao, kupitia mradi huo, VETA imenunua vifaa
vyenye thamani ya zaidi ya milioni 30,250,000, vikiwemo vyerehani 70; vifaa kwa
ajili ya mafunzo ya urembo (saluni) na vifaa kwa ajili ya mafunzo ya umeme.
Mabelele amesema
kutokana na ununuzi wa vifaa katika chuo hicho, VETA imepanga kuanzisha kozi za
muda mrefu katika fani za Ushonaji, Ubunifu wa Mavazi na Teknolojia ya Nguo na
Ufundi umeme, ambazo zitaanza kutolewa Januari 2024.
“Kupitia mradi huu wa “Chaguo langu haki
yangu” vijana hawa wameweza kubadilishiwa mtazamo wa kimaisha hasa katika jamii
wanapokwenda, kwani tayari wana uwezo wa kuajiriwa au kujiajiri,” Ameongeza.
Naye Mkurugenzi wa
Shirika la wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika WiDAF Bi. Anna Kulaya
amesema, kuhitimu kwa mabinti hao kunatoa hamasa kwa shirika lake kuendelea
kutafuta wafadhili wengine zaidi ili kusaidia mabinti wengi zaidi kuweza kupata
fursa ya kupata mafunzo ya ufundi stadi.
Amesema kuwa kupita
mafunzo hayo, mabinti wengi wameweza kufufua ndoto zao na kupata matumaini
mapya ya maisha na kuongeza kuwa anaamini mabinti hao wanaweza kujiajiri au
kuajiriwa na pengine kufungua biashara zao mbalimbali ikiwemo kwenye upishi na
biashara ndogo ndogo.
Baadhi ya wanafunzi
wahitimu wa mradi huo wamepongeza na kushukuru kupata mafunzo hayo na kuahidi
kwenda kuwa mabalozi katika jamii zinazowazunguka.
“Mimi nimejifunza kitu kikubwa sana kupitia
mafunzo haya, nina hakika nikitoka hapa ninaenda kujitegemea mwenyewe na
sitakuwa tegemezi kama ilivyokuwa kipindi cha awali,” Amesema Naomi Jonas,
Mhitimu katika fani ya Ufundi Bomba.
Awamu ya kwanza ya mradi wa Chaguo Langu Haki Yangu” ilitekelezwa katika mikoa ya Mara na Shinyanga, wilaya za Kahama, Butiama na Kishapu.
No comments:
Post a Comment