CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Tuesday 12 September 2023

Chuo cha VETA Ndolage kinatarajiwa kuongezewa hadhi ya kuwa chuo cha VETA cha wilaya ya Muleba.

 Rai hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Dkt. Franklin Rwezimula, tarehe 11.09.2023 alipotembelea chuo cha VETA-Ndolage kwa lengo la kukagua na kujionea ujenzi unaoendelea katika chuo hicho.


Katika ziara hiyo Dkt.Rwezimula alikagua Ujenzi wa jumla ya majengo 6, ambayo ni jengo la karakana ya umeme wa majumbani, bwalo la chakula lenye uwezo wa kuhudumia watu 200 kwa mkupuo, nyumba ya mkuu wa chuo, jiko na mabweni mawili ya wanafunzi wa kike na kiume yenye uwezo wa kubeba jumla ya wanafunzi 160.

Dkt Rwezimula aliongeza kuwa upanuzi wa chuo cha VETA-Ndolage utakaokipandisha hadhi chuo hicho kutoka kuwa VTC na kuwa DVTC ni sehemu pia ya utekelezaji wa mpango  Serikali ya awamu ya Sita ya kuhusu utoaji  Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi ili kuzalisha nguvu kazi yenye Ujuzi utakaowawezesha vijana  kujiajiri au kuajiriwa.

Akisoma ripoti ya uendelezaji wa ujenzi, Kaimu Mkuu wa chuo cha VETA-Ndolage, Machumu Kingi Machumu amesema shilingi milioni 903.57 zilitengwa na serikali kwa ajili ya kazi ya upanuzi wa chuo hicho, ambapo mpaka sasa zimetumika shilingi milioni 189.1.


Kumalizika kwa  utekelezaji wa upanuzi wa chuo VETA-Ndolage kunatarajiwa kuleta ongezeko la udahili kutoka wanafunzi 70 wa mwaka huu 2023 na kufikia wanafunzi 200 ambapo 160 watapata nafasi ya kukaa bweni na 40 kutwa. 

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema upanuzi huo utahitaji ongezeko la walimu ili kukidhi utoaji Mafunzo, hivyo VETA imejiandaa kuomba vibali vya kuajiri huku akiahidi kutumia walimu wa muda  kutoka vyuo vya jirani kusaidia kutoa mafunzo.

Amesema, utekelezaji wa Upanuzi  wa chuo cha VETA-Ndolage utakwenda sambamba  na ongezeko la kozi za Ufundi Magari, Ufundi Umeme wa Magari, Udereva wa Magari  na pikipiki, kozi ya


Uongezaji thamani Mazao ya Chakula ili kuhakikishia wananchi wa Muleba wanapata nguvu kazi yenye ujuzi kwa ajili ya uzalishaji wenye tija.

Chuo cha VETA-Ndolage kilianza kutoa mafunzo Juni 2020 kwenye fani za Uashi, Uundaji na Uungaji vyuma, Uhazili na Kompyuta pamoja na Ushonaji, Ubunifu wa Mavazi na Teknolojia ya Nguo.

No comments:

Post a Comment