CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Sunday 24 September 2023

MILIONI 900 KUTUMIKA KUPANUA CHUO CHA VETA NDOLAGE


Serikali imetenga kiashi cha Shilingi 903,577,628 kwa ajili ya kujenga na kuongeza majengo na miundombinu ya Chuo cha Ufundi Stadi Ndolage, kilichopo wilaya ya Muleba, mkoani Kagera ili kuongeza udahili na kuweka mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia katika chuo hicho.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Kasore, wakati akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa uboreshaji wa chuo hicho kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, alipotembelea na kukagua chuo hicho leo, tarehe 24 Septemba 2023.

CPA Kasore amesema, uamuzi huo umechukuliwa kwa kuzingatia uchache wa miundombinu ya chuo hicho na uwezo wake mdogo katika kukidhi mahitaji ya wananchi katika wilaya ya Muleba na maeneo ya jirani.

Amesema Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi inatekeleza mradi wa uboreshaji wa chuo hiki kwa kutumia utaratibu wa nguvukazi ya ndani, yaani Force Account. 

Amesema uboreshaji wa chuo unahusisha ujenzi wa bweni la wavulana lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80; bweni la wasichana lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80; bwalo la chakula lenye uwezo wa kuhudumia watu 200; karakana ya Umeme; karakana ya Uungaji na Uundaji vyuma; nyumba ya Mkuu wa Chuo na jengo la jiko.

“Uboreshaji wa Chuo hiki utawezesha kuanza kudahili wanafunzi wa bweni, ambapo chuo kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi wa 160, kati yao 80 wa kike na 80 wa kiume. Pia kuongeza udahili wa wanafunzi 40 wa fani ya umeme ambayo karakana yake inajengwa sasa,” amesema.

Baada ya kupokea taarifa na kutembelea majengo ya chuo hicho, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa ameipongeza VETA kwa kuendelea kusimamia na kutekeleza vyema ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi unaoendelea katika maeneo mbalimbali nchini.

"Nimepita maeneo mengi, Chunya, Newala, Tabora, Ruangwa, …kote huko naona VETA mnafanya kazi nzuri sana. Hongereni sana, endeleeni kufanya vizuri,” amesema.

Amesema ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi nchini ni mkakati muhimu wa Serikali kuhakikisha wananchi wanapata ujuzi wa kuwawezesha kunufaika kiuchumi wao binafsi na kuchangia kwenye maendeleo ya nchi.

Amewahamasisha wananchi kutumia vyema fursa pana za mafunzo ya ufundi stadi ili kujipatia ujuzi kwa manufaa yao.

Chuo hicho kilianza kutoa mafunzo rasmi mwezi Juni, 2020 katika fani nne, ambazo ni Uashi; Uungaji na Uundaji Vyuma; Uhazili na Ubunifu wa Mavazi, Ushonaji na Teknolojia ya Nguo. Hata hivyo, kutokana na upungufu wa miundombinu, chuo hicho bado kina uwezo mdogo wa kudahili, ukilinganisha na mahitaji ya wananchi wa Wilaya ya Muleba na maeneo ya jirani.




No comments:

Post a Comment