CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Saturday 14 October 2023

MAPENDEKEZO YA MUUNDO WA ELIMU NA MABADILIKO KATIKA MITAALA YAWASILISHWA KWA BODI NA MENEJIMENTI YA VETA

 

Taasisi ya Elimu Tanzania (TET),


tarehe, 13 Oktoba 2023 imewasilisha mapendekezo ya muundo wa elimu na mabadiliko yaliyopo kwenye Rasimu ya mitaala mipya ya elimu kwa Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).

Wasilisho hilo limefanyika katika chuo cha VETA cha Hoteli na Utalii (VHTTI), Njiro, jijini Arusha.

Akizungumza kwenye tukio hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba, amesema lengo la wasilisho hilo ni kuwapatia ufahamu Bodi na Menejimenti ya VETA kuhusu utekelezaji wa elimu ya Amali kwa Sekondari Hatua ya Chini, ambapo utekelezaji wake kwa kiasi kikubwa utafanywa na kusimamiwa na VETA


Dkt. Aneth Komba amefanya wasilisho hilo mbele ya mwenyekiti wa Bodi hiyo, Prof. Sifuni Mchome, wajumbe wa Bodi pamoja na Menejimenti ya VETA.

Ameeleza kuwa mitaala mipya itasaidia katika kumuandaa mwanafunzi kujitegemea, kwani atakuwa na uwezo mzuri kutokana na ujuzi atakaopata kupitia mabadiliko hayo ya elimu.

"Maboresho haya ya Mitaala mipya ya elimu yamefanyika kwa kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha elimu itakayomuwezesha mhitimu kujiajiri au kuajiriwa baada ya kumaliza masomo yake, " amesema Dkt.Komba.

Baada ya uwasilishaji, Dkt.Komba amekabidhi taarifa mbalimbali zilizofanyiwa kazi kwa VETA kupitia nakala laini (soft copy), ili kuwezesha utekelezaji wa rasimu ya mitaala.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya VETA, Prof Mchome, ameeleza kuwa wasilisho la Mitaala ni jambo jema, kwani itawasaidia wajumbe wa Bodi na Menejimenti nzima ya VETA kupata uelewa na kuwawezesha kujipanga katika utekelezaji wa mabadiliko hayo.

"Matarajio kwa wananchi ni makubwa kwenye maboresho ya mitaala hii, hivyo ni wazi kuwa sasa kazi itaanza vyema ya kuhakikisha elimu imeboreshwa na kwamba sasa tunapaswa kujipanga vyema kama VETA,” amesema.

Katika kikao hicho, wajumbe wa Bodi na Menejimenti ya VETA, wameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na TET kwa kazi kubwa ya maboresho ya Mitaala na kuahidi kusimamia utekelezaji na kutekeleza kwa umahiri katika maeneo yanayoigusa VETA.


No comments:

Post a Comment