CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Sunday 15 October 2023

Prof. Mchome ahimiza utatu katika kufikia malengo ya VETA

 

Kikao cha kwanza cha Bodi ya Tisa ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VET Board) kimehitimishwa, tarehe 14 Oktoba 2023, jijini Arusha, huku Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Sifuni Mchome akihimiza utatu wa Bodi, Menejimenti na Watumishi katika kutekeleza majukumu ya VETA.

Katika kikao hicho kilichofanyika kwenye Chuo cha VETA cha Hoteli na Utalii, Njiro, jijini Arusha, Profesa Mchome amesema kuwa Bodi inatakiwa kutoa maelekezo sahihi, Menejimenti ya VETA kuanda miongozo na kuweka mikakati thabiti ya utekelezaji na wafanyakazi kujitoa kwa dhati katika kutekeleza majukumu mbalimbali.

“Sisi tunachotaka ni kufanya kazi kwa utatu ili kufikia malengo…Katika utatu huo, Watumishi wasiiangushe Menejimenti, Menejimenti isiiangushe Bodi na Bodi itatoa maelekezo sahihi ya kitu cha kufanya… ule utatu ukitimia basi tutaweza kufikia malengo”, amesema.

Ameitaka Menejimenti ya VETA kutambua na kuichambua miradi ya Kimkakati iliyopangwa au inayotekelezwa na Serikali, kisha kubuni programu mbalimbali za mafunzo ili kujibu mahitaji ya ujuzi katika miradi hiyo.


Prof. Mchome amesema miongoni mwa mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuwapatia wananchi ujuzi ambao ndiyo msingi mkuu katika kuwawezesha kushiriki katika uchumi wa sasa wa dunia na kusisitiza kuwa VETA inategemewa zaidi katika kufanikisha mkakati huo.

“Nchi inahitaji ujuzi unaoendana na maendeleo ya kidunia na VETA ndiyo chombo cha kubaini na kutekeleza mahitaji hayo,” amesema. Akizungumzia Sera mpya ya Elimu na mabadiliko katika mitaala ya Elimu, Profesa Mchome amesema, VETA inategemewa kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa mitaala mipya ya sekondari, kwani mwelekeo wa mitaala hiyo ni mafunzo ya ujuzi. Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore ameishukuru Bodi mpya kwa kuanza vyema katika kupanga utekelezaji wa majukumu yake na kuahidi kwa niaba ya Menejimenti ya VETA kutekeleza maelekezo na miongozo mbalimbali itakayotolewa na Bodi.


Bodi ya Tisa ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi inayowahusisha wajumbe kutoka taasisi za Serikali, sekta binafsi, waajiri, waajiriwa na taasisi za dini ilianza kikao chake kwa kufanya kikao kazi cha kueleweshana na kujengeana uwezo kuhusu utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Mamlaka.

No comments:

Post a Comment