Makampuni ya Kimataifa ya Shell na
Equinor yameunga mkono juhudi za Serikali kuwezesha vijana kupata ujuzi na
kuongeza fursa za kuajirika kwa kutoa ufadhili kwa vijana 24 mkoani Lindi
kujifunza fani mbalimbali za ufundi stadi Ngazi ya Tatu (Level 3).
Ufadhili wa makampuni hayo umehusisha ada, bima ya afya, malazi, chakula, usafiri pamoja kutoa vitendea kazi kwa wahitimu ili kuwawezesha kujiajiri mara baada ya kuhitimu mafunzo.
Akizungumza wakati wa mahafali ya wahitimu ya wahitimu hao, yaliyofanyika tarehe 13 Oktoba, 2023 kwenye Chuo cha VETA Lindi, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga, aliyemwakilisha Mkuu wa mkoa wa Lindi, alisema ufadhili huo umelenga kuwaandaa wahitimu hao kuweza kujiajiri pamoja na kupata nguvu kazi yenye ujuzi utakaotumika katika miradi ya Kimkakati ya Gesi mkoani Lindi.
Ndemanga aliyashukuru makampuni hayo kwa kufadhili mafunzo na kuwaomba kupanua wigo wa ufadhili huo kwa wanafunzi wa ngazi ya kwanza na ya pili.
Aliwasihi wahitimu kwenda kujiunga katika vikundi ili kuwarahisishia kupata mikopo itakayowasaidia kuendeleza miradi ya uzalishaji.
Akisoma taarifa ya chuo kwa mgeni rasmi, Kaimu Mkuu wa Chuo cha VETA Lindi, Harry Mmari, alisema mafunzo hayo yamechukua muda wa mwaka mmoja, ambapo vijana walipata ufadhili kwa asilimia 100 kwa kulipiwa ada, bima ya afya, malazi, chakula, usafiri pamoja na kupatiwa vitendea kazi vya kwenda kujiajiri mara baada ya kuhitimu na kufaulu mafunzo yao.
No comments:
Post a Comment