CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Wednesday 4 October 2023

VETA YAWEZESHA MAFUNZO KWA WATUMISHI 40 WANAOJIANDAA KUSTAAFU

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kupitia Chuo cha Utumishi wa Umma imetoa mafunzo kwa watumishi wanaotarajia kustaafu katika kipindi cha mwezi Novemba, 2023 hadi Oktoba, 2024.

Akifungua mafunzo hayo ya siku nne jijini Dodoma tarehe 3 Oktoba, 2023, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwaandaa watumishi hao na maisha baada ya kustaafu na kuwawezesha kujiwekea mipango sahihi ili kuyamudu vyema maisha nje ya Utumishi wa Umma.

“Tumeona kuna umuhimu wa kukumbushana masuala mbalimbali ya msingi ili maisha ya kustaafu yawe mazuri…baada ya kustaafu ni muda mzuri wa kufanya mambo mengi zaidi,” amesema.

CPA Kasore amewasihi watumishi hao kuendelea kutoa mchango wao hasa katika kuishauri Mamlaka katika masuala mbalimbali ya kuongeza ufanisi katika utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi.

Aliwasisitiza pia umuhimu wa kuhakiki taarifa za michango yao katika mifuko ya jamii na kuweka na kuandaa nyaraka zao mbalimbali kusaidia ufuatiliaji wa mafao.

Mkurugenzi wa Rasilimaliwatu na Utawala wa VETA, Ndg. Felix Staki, amesema Mamlaka inajipanga kuhakikisha mafunzo hayo yanatolewa mapema zaidi ili kuwawezesha watumishi kujiandaa mapema na maisha baada ya kustaafu. 

Ndg. Staki amebainisha kuwa washiriki watajifunza masuala mbalimbali ikiwemo ujasiriamali, uwekezaji, usimamizi wa fedha, uendeshaji wa biashara na afya.

Akitoa shukrani zake kwa niaba ya watumishi wengine wanaotarajia kustaafu, Mkuu wa Chuo cha VETA Mtwara, Ndg. Joseph Kibehele, amesema mafunzo hayo yatawanufaisha na kuahidi kuyazingatia ili kuishi vizuri baada ya kuhitimisha utumishi wa umma.




No comments:

Post a Comment