CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Friday 27 October 2023

Wahitimu 119 wa VETA wapatiwa mitaji kuwawezesha kujiajiri

Jumla ya vijana 119 waliohitimu mafunzo ya ufundi stadi chini ya Mradi wa Kukuza Ajira na Ujuzi kwa Maendeleo Tanzania (E4DT) wamepatiwa mitaji mbegu ya vitendea kazi ili kuwawezesha kujiajiri. 

Wahitimu hao ni washindi wa shindano la mtaji mbegu lililoandaliwa na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Uongozi na Ujasiriamali (IMED Foundation) na kufadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Korea (KOICA) kupitia mradi wa E4DT ulioanza kutekelezwa mwezi Mei, 2022, ukilenga kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa vijana 4000 nchini, katika fani za  Ufundi Bomba  wa majumbani, Ufundi Bomba viwandani, Ufundi wa Uchomeleaji vyuma viwandani na Ufundi wa Mekatroniki katika vyuo vya VETA vya Dodoma, Lindi, Manyara na Kipawa kwa lengo la kukuza ajira kwa vijana.

Akikabidhi vifaa hivyo kwenye hafla iliyofanyika katika Chuo cha VETA Dodoma, tarehe 27 Oktoba, 2023, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mhe. Godwin Gondwe, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma amepongeza hatua hiyo inayolenga kutatua changamoto za ajira kwa vijana. 

Mhe. Gondwe ameipongeza VETA na wadau walioshiriki kuwajengea uwezo vijana hao katika stadi za ufundi na ujasiriamali na kwamba itawasaidia kujiajiri na kuajiri vijana wenzao.

 “Kazi inayofanywa na VETA ya kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi inaendana na Dira ya Taifa na mipango ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo Serikali inafanya jitihada nyingi kuweka mazingira wezeshi na kujenga uwezo wa vijana kujiajiri,”amesema

Amewataka vijana hao kutumia vifaa hivyo walivyovipata kuendesha shughuli zao kwa ufanisi kwa kuzingatia nidhamu na uadilifu ili kufikia malengo yao, pamoja na kutumia vyema mitandao ya kijamii kutangaza shughuli zao.

 “Nawasihi sana kuwa na nidhamu, uadilifu, utunzaji muda, lugha nzuri na kutimiza ahadi zenu kwa wateja… Tumieni vyema pia mitandao ya kijamii kutangaza biashara zenu,”amesema

Mkurugenzi Mtendaji wa IMED Foundation, Swabiri Khalidi amesema awamu ya kwanza ya mafunzo ya ujasiriamali ilihusisha wanagenzi 251, waliowasilisha jumla ya maandiko ya miradi 50 yakihusisha wanagenzi 143 kuomba mtaji mbegu, ambapo miradi 40 yenye wanagenzi 119 iliibuka washindi.

Amesema washindi hao wataingizwa katika huduma za uatamizi wa biashara kwa muda wa kati ya miezi mitatu hadi sita ambapo watapatiwa huduma za ushauri wa biashara na mafunzo ya uendeshaji wa biashara ili waweze kusimamia imara biashara zao na kuzifanya kuwa endelevu.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema VETA inajivunia mafanikio yaliyopatikana kupitia mradi huo ikiwemo mafunzo kwa walimu na maboresho ya karakana na vifaa vilivyopatikana ambavyo vitaendelea kuwezesha utoaji mafunzo ya ufundi stadi kwa ufanisi.

Mkurugenzi Mkazi wa KOICA Tanzania, Ndg. Man Shik SHIN amesema Serikali ya Korea inaamini katika kuwapatia ujuzi vijana, hasa kwa kutambua mchango wao katika maendeleo ya nchi kiuchumi.

Amesema ufadhili wa mafunzo ya ujuzi na ujasiriamali na utoaji wa vifaa vya kazi kwa vijana hao utawawezesha kujiajiri na kufikia malengo waliyojiwekea.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wanagenzi wanufaika wa mradi wa mtaji mbegu, Bi. Olga Chomola amesema vifaa hivyo vitawasaidia kujiajiri na kuajiri vijana wenzao na kuiomba VETA na wadau kuendelea kuwezesha ujuzi kwa vijana.




No comments:

Post a Comment