Bodi ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Stadi imemteua Dkt. Prosper Lutangilo Mgaya kuwa Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
Dkt. Mgaya anachukua nafasi ya Dkt. Pancras Bujulu ambaye alistaafu utumishi wa umma mwezi Machi, 2022 na nafasi hiyo kukaimiwa na CPA Anthony Kasore ambaye ni Mkurugenzi wa Fedha wa VETA. Uteuzi wa Dkt. Mgaya ni kuanzia tarehe 1 Novemba, 2023. Kabla ya Uteuzi huo Mgaya, alikuwa Naibu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) upande wa Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi.
Akizungumza na
wafanyakazi wa VETA Makao Makuu katika ofisi za Mamlaka hiyo jijini Dodoma
alipowasili rasmi leo tarehe 6 Novemba, 2023, Dkt. Mgaya amesisitiza dhamira
yake ya kuhakikisha malengo ya Serikali ya kutoa ujuzi kwa Watanzania kupitia
vyuo vya VETA nchini yanafikiwa.
Amesema Serikali
imewekeza nguvu kubwa katika kuhakikisha vyuo vya VETA vinakuwa karibu zaidi na
wananchi ili watanzania wa ngazi zote waweze kujipatia ujuzi hivyo VETA ina
jukumu la kuweka mipango na mikakati thabiti katika kufanikisha dhamira hiyo ya
Serikali.
Dkt. Mgaya amewataka wafanyakazi wa VETA kufanya kazi kwa bidii na weledi na kuwasihi kumpatia ushirikiano katika kufanikisha malengo ya Mamlaka hiyo na mategemeo ya Serikali.
Amewasihi wafanyakazi
kufanya kazi kwa ushirikiano na kutambua umuhimu wa mchango wa kila mmoja
katika kufikia malengo ya taasisi.
''Kila mmoja ana sifa zake ambazo Mungu amemkirimia kuweza kuisaidia VETA kusonga mbele. Ni juu ya viongozi kuangalia nani mzuri kwenye eneo gani na asaidie wapi?''amesema.
Ameongeza kuwa yeye kama kiongozi aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa VETA, hana ufumbuzi wa kila changamoto aliyoikuta, bali ushirikiano wa pamoja miongoni mwa wafanyakazi ndio utakaowezesha kutatua kutafuta ufumbuzi wa kutatua changamoto na kusonga mbele.
Awali Mkurugenzi wa Fedha wa VETA aliyekuwa akikaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu, CPA Anthony Kasore amempongeza Dkt. Mgaya kwa kuteuliwa na kueleza imani yake kwa Dkt. Mgaya katika kufanya mageuzi ndani ya VETA hasa kwa kuzingatia kuwa amebobea na ana uzoefu wa kutosha kwenye eneo la ufundi.
CPA Kasore amewasihi watumishi wa VETA kumuunga mkono Mkurugenzi Mkuu huyo mpya kwa kutimiza wajibu wao kwa uaminifu na ufanisi ili kuleta mafanikio kwenye Taasisi hiyo.
Akimkaribisha na kutoa neno la shukrani kwa niaba ya watumishi wa VETA, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi VETA Makao Makuu, Ndg. Christopher Msigwa amempongeza Dkt. Mgaya kwa kuteuliwa kuiongoza VETA na kumtakia utendaji kazi bora katika nafasi yake.
Dkt. Mgaya ni
Mhandisi mbobevu katika masuala ya Rasilimali Maji (Water Resources
Engineering). Amekuwa kwenye utumishi wa umma akiwa mhadhiri na akishika nafasi
mbalimbali za uongozi katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Chuo
cha Taifa cha Usafirishaji (NIT). Vilevile, Dkt Mgaya ni Mwenyekiti wa Bodi ya
Sayansi na Teknolojia Shirikishi (Science and Allied Technologies) ya Baraza la
Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET). Pia ameshika nafasi
mbalimbali za usimamizi,utafiti na ushauri elekezi kwenye taasisi na miradi
mbalimbali.
No comments:
Post a Comment