Wahitimu wa kidato
cha nne wahamasishwa kujiunga na kozi za muda mfupi kwenye vyuo vya VETA
Mamlaka ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) inashiriki kwenye maonesho ya Maadhimisho ya
Miaka 50 ya Baraza la Mitihani la Tanzania(NECTA), yanayofanyika katika viwanja
vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Novemba hadi 3 Desemba, 2023.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amefungua rasmi maonesho hayo leo tarehe 30 Novemba, 2023, ambapo viongozi mbalimbali wakiwepo Wakuu wa Taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pia wamehudhuria.
Mkurugenzi wa VETA
Kanda ya Dar es Salaam, Ndg. Angelus Ngonyani, amemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa
VETA kwenye hafla ya ufunguzi, akiambatana na Mkuu wa Chuo cha VETA Dar es Salaam,
Mhandisi Joseph Mwanda.
VETA inatumia
maonesho hayo kutoa taarifa mbalimbali za mafunzo ya ufundi stadi yanayotolewa
kwenye vyuo vyake na kuhamasisha wananchi, hasa wahitimu wa kidato cha nne
mwaka huu, kujiunga na kozi za muda mfupi, katika kipindi cha mpito kabla ya
matokeo na/au kuendelea na ngazi zingine za masomo. Mafunzo hayo
yatawasaidia kuwa na hazina ya ujuzi
unaowawezesha kuajirika kwa urahisi.
Kupitia maonesho hayo
pia VETA inawaelimisha wananchi namna ilivyojipanga katika kuwezesha utoaji wa
mafunzo ya amali kuendana na mabadiliko
ya mitaala ya elimu ya Sekondari.
VETA inawakaribisha
wananchi wote kutembelea banda lake kwenye maonesho hayo ili kupata taarifa
mbalimbali zinazohusu mafunzo ya ufundi stadi na kujionea kwa uhalisia shughuli
za mafunzo.
No comments:
Post a Comment