Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii,
imepongeza utoaji mafunzo ya uanagenzi katika chuo cha VETA Mwanza, kupitia
ufadhili wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
Pongezi hizo zimetolewa Jijini Mwanza, tarehe 19 Machi, 2024,
wakati wa ziara ya Kamati hiyo kukagua utekelezaji wa mafunzo ya ukuzaji ujuzi
kwa njia ya Uanagenzi katika chuo cha VETA Mwanza.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Fatuma Hassan Toufiq, amesema
kazi kubwa ya kamati yake ni kuangalia na kukagua utekelezaji wa miradi ambayo
Serikali imetoa fedha ili kuona thamani ya fedha katika miradi hiyo.
“Katika chuo hiki
tumefarijika sana kuona vijana mbalimbali wakipatiwa mafunzo…tumepita katika
karakana tumejionea vijana wa kike na kiume wakijifunza namna ya kuwa mafundi
wa aina mbalimbali kama vile mafundi bomba, mafundi umeme, useremala na wengine
wengi,” amesema.
Wakiwa kwenye karakana za mafunzo, wajumbe hao waliwapongeza
vijana kwa umahiri wa kuonesha na kuelezea kile walichojifunza na bidhaa mbalimbali
walizozalisha kutokana na mafunzo.
Mhe. Toufiq amewataka vijana waliopata mafunzo ya kukuza
ujuzi kwa njia ya uanagenzi katika chuo cha VETA Mwanza kuhakikisha wanatumia
vyema ujuzi wao ili kuwaletea tija katika shughuli zinazohusiana na ufundi
stadi, hivyo kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.
Amesema Kamati hiyo itaishauri Serikali kuona uwezekano wa
kuwawezesha wahitimu wa programu hiyo vifaa vya kufanyia kazi ili waweze
kujiajiri.
Naye Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira
na Wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja, amesema programu ya ukuzaji ujuzi
kwa njia ya uanagenzi imelenga kuwezesha nguvukazi ya Taifa, hususani iliyopo
katika soko la ajira, kupata ujuzi na stadi za kazi stahiki ili iweze
kujiajiiri au kuajiriwa.
Amesema jumla ya shilingi bilioni 2.7 zimetengwa ili
kuwezesha utekelezaji wa programu kwa vijana 6000 wakiwemo wenye ulemavu 84.
Katika chuo cha VETA Mwanza jumla ya wanafunzi 132 (wanaume
102 na wanawake 30) wanaendelea na mafunzo katika fani za Useremala, Uashi, Upakaji
rangi, Ufundi Mashine za kuchakata Pamba, Ufundi Bomba, Umeme wa Majumbani,
Ufundi Magari, Upishi na Uchomeleaji na Uungaji Vyuma.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Antony Kasore, VETA imeanzisha programu
mbalimbali ambazo zinawasaidia wananchi wa Kitanzania kupata ujuzi na kufanya
shughuli mbalimbali ambazo zitawaingizia kipato.
Baadhi ya vijana wanaopata mafunzo hayo, wameipongeza
Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa
kuwapatia fursa hiyo muhimu na kusema baada ya mafunzo hayo wanatarajia
kujiajiri ili kuweza kujikimu katika maisha yao.
Aidha, wanafunzi hao wameiomba Serikali kuwasaidia vifaa vya
kazi za ufundi stadi kwa fani mbalimbali walizojifunza ili utekelezaji wa
shughuli hizo baada ya kuhitimu uweze kufanikiwa.
No comments:
Post a Comment