Mwenyekiti wa Bodi ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Prof. Sifuni Mchome, ameiagiza Mamlaka ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kuongeza kasi ya uzalishaji wa bidhaa
mbalimbali za kiubunifu ili kutatua changamoto za wananchi na kuzalisha kipato.
Prof. Mchome ametoa
maagizo hayo tarehe 30 Mei, 2024 jijini Tanga alipotembelea banda la VETA
kwenye Maadhimisho ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayofanyika jijini
humo.
Amesema walimu na
wanafunzi wa vyuo vya VETA nchini wanafanya kazi nyingi za kiubunifu ambazo
zinahitajika kwa wingi katika kuongeza ufanisi kwenye shughuli za uzalishaji
zinazofanywa na wananchi lakini bidhaa hizo za kiubunifu hazijaweza kuzalishwa
kwa wingi na kuwafikia wahitaji.
“Kwa kweli
nimeridhika sana na ubunifu unaofanyika na vitu mbalimbali vinavyozalishwa
kupitia VETA … sehemu zote nilizopita unaona ni vitu vinavyoenda kusuluhisha
changamoto mbalimbali za watanzania lakini changamoto ni kuvizalisha kwa wingi
ili vifike sokoni,”amesema.
Prof Mchome amesema
ni wajibu wa VETA kutoa mafunzo ya ufundi stadi na kuwajengea ujuzi Watanzania
pamoja na kutumia wabunifu wake kuzalisha bidhaa zitakozowawezesha kujipatia
kipato kuanzia kwa mwanafunzi, mwalimu na taasisi kwa ujumla.
“Ujumbe wangu ambao
nimekuwa nikiutoa sehemu zote ni kuwa tutengeneze pesa kwa kuwa kazi ya ujuzi
ni kazi ya kuzalisha vitu vinavyohitajika kwenye soko la kitaifa na kimataifa
na kufanya biashara kupitia vitu hivyo,” amesema
Prof. Mchome
amewahamasisha wanafunzi na walimu wa VETA kuwa na mtazamo wa biashara ili
wanapobuni vitu mbalimbali waweke msukumo katika kuvizalisha kwa wingi.
Kwa mujibu wa Prof.
Mchome, mtazamo wa kibiashara utawezesha wahitimu wa VETA kujikita katika
kuanzisha makampuni na kuzalisha bidhaa mbalimbali kutokana na mafunzo na fikra
za kibiashara walizojengewa tangu wanapojiunga na vyuo vya VETA.
No comments:
Post a Comment