Kiongozi wa Mbio za
Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2024, Ndugu Godfrey Eliakimu Mnzava, jana, tarehe
9 Juni, 2024 ameweka Jiwe la Msingi katika mradi wa ujenzi wa
mabweni mawili chuo cha ufundi stadi cha VETA Wilaya ya Namtumbo unaojengwa kwa
kutumia nguvukazi ya ndani (force account).
Ujenzi wa mradi huo
unaokadiriwa kugharimu shilingi milioni
800 umefikia asilimia 85.
Jiwe hilo la msingi
limewekwa baada ya viongozi wa mbio za
Mwenge kujiridhisha kuwa mradi huo umekidhi viwango vya ujenzi kwa
mujibu wa miongozo ya ujenzi wa majengo ya Serikali.
"Mwenge wa Uhuru umefanya ukaguzi wa kina kuhusu nyaraka zinazohusiana na mradi, umetembelea na kujionea miundombinu ujenzi ulipofikia. Tunafanya haya ili kuhakikisha tunabaini ubora na viwango vinavyotakiwa katika mradi husika, thamani ya fedha iliyotumika kama inaakisi maendeleo na uhalisia wa matokeo ya mradi," amesema Mnzava.
Naye, Mkuu wa wilaya
ya Namtumbo Mheshimiwa Ngollo Malenya amesema Mradi wa ujenzi wa mabweni hayo
utaongeza idadi ya wanafunzi chuoni hapo kwani
utasaidia katika kutatua changamoto ya wanafunzi wenye nia ya kusoma
lakini wanatoka mbali na chuo.
Akitoa taarifa kuhusu
ujenzi wa mradi mabweni hayo, Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Privatus Majiyamotoo
amesema mradi huo hadi sasa umefikia zaidi ya asilimia 85 katika ujenzi wake
ambapo hadi kukamilika unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi mil 800 ambapo chanzo cha fedha hizo ni Serikali kuu.
No comments:
Post a Comment