CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Wednesday 19 June 2024

WASIMAMIZI WA VYUO VIPYA VYA VETA WAJENGEWA UWEZO UENDESHAJI WA MAFUNZO YA UFUNDI STADI KWA UFANISI

 

Jumla ya wasimamizi wa vyuo vipya vya VETA wamejengewa uwezo wa uratibu na uendeshaji wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi ili kuimairisha utoaji mafunzo na kuzalisha wahitimu mahiri.

Kikao kazi cha kujengeana uwezo kinafanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 18 hadi 19 Juni 2024 katika ukumbi wa Chuo cha VETA Dodoma na kimefunguliwa leo, tarehe 18 Juni, 2024 na Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dkt.Abdallah Ngodu aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa VETA.

Dkt. Ngodu amewahimiza washiriki hao kufuatilia kwa makini mada mbalimbali zilizoandaliwa ambazo zitawawezesha kufanya kazi kwa ufanisi na kuhakikisha malengo ya VETA yanafikiwa.

“tumekutana hapa kwa ajili ya kukumbushana na kuelekezana misingi tunayopaswa kuifuata na kuiheshimu katika kuhakikisha kazi ya utoaji mafunzo kwa ajili ya kuzalisha Watanzania wenye ujuzi, hasa vijana mnaowahudumia katika vituo vyenu inatekelezwa kwa ufanisi,” amesema.

Afisa Mkuza Mitaala wa VETA, Bi. Happiness Salema, amesema kikao kazi hicho ni sehemu muhimu ya kupeana mrejesho wa utekelezaji wa shughuli za utoaji mafunzo kwenye vyuo vya VETA na kubadilishana uzoefu ili hatimaye kuleta weledi katika utoaji mafunzo.

Mwakilishi wa wasimamizi wa vyuo vinavyoshiriki, ambaye ni Kaimu Msajili wa Chuo cha VETA cha Wilaya ya Ukerewe, Mhandisi Shinzeh Deudedith, ameshukuru uongozi wa VETA kwa kuandaa kikao kazi hicho na kuahidi kuyafanyia kazi mafunzo na maelekezo watakayoyapata.

Kikao kazi hicho kinahusisha Wasimamizi wa Vyuo vipya 30 ambapo, 26 wanatoka vyuo vya ngazi ya Wilaya na wanne (4) kutoka vyuo vya ngazi ya Mkoa ambapo mada zitakazowasilishwa ni pamoja na utekelezaji wa Mitaala, miongozo mbalimbali ya utoaji wa mafunzo ikiwa ni pamoja na Ufuatiliaji na Tathmini, Mafunzo ya Uanagenzi kwa Mfumo Rasmi, Uchaguzi wa Wanafunzi, Unasihi na Ushauri wa Mafunzo na Kazi,Elimu Jumuishi ya Wanafunzi wenye Mahitaji Maalum na Uendeshaji na Tathmini ya Mitihani.Mada nyingine zitakazowasilishwa ni pamoja na Upangiliaji Karakana na Utangazaji wa fursa za Mafunzo.

No comments:

Post a Comment