Mamlaka ya Elimu na
Mafunzo Ya Ufundi Stadi (VETA) na Tanzania House of Talents (THT) zimetia saini
hati ya makubaliano, kuanzisha ushirikiano wa kutoa mafunzo katika sekta ya
sanaa ili kuwawezesha vijana kuwa na ujuzi unaotambulika rasmi katika sekta hiyo
hapa nchini.
Makubalioano hayo
yamesainiwa tarehe 25 Julai 2024 na
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore na Mkurugenzi Mkuu wa THT
Kemilembe Mutahaba, katika ukumbi wa mikutano, VETA Makao Makuu, Jijini Dodoma.
Akizungumza kabla ya
utiaji saini wa hati hiyo ya ushirikiano, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Kasore
amesema sambamba na juhudi ilizoanzisha zikilenga kuboresha sekta ya sanaa
nchini, VETA imeona ni vyema kuanzisha ushirikiano na wadau muhimu katika sekta
hiyo ili ujengeaji ujuzi kwa vijana uwe wenye matokeo makubwa zaidi.
Amezitaja juhudi
zilizofanywa na VETA kwa nia ya kuboresha sekta ya sanaa nchini kuwa ni pamoja
na kuandaa mitaala mipya ya ikiwemo ya Utengenezaji wa Filamu (Film
Production), Sanaa na Usanifu (Arts and Design), Uandaaji wa Matukio (Events
Planning) na Uandaaji Muziki (Music Production).
“THT wako na vijana kwa
muda mrefu, wanawafundisha na kukuza vipaji vyao katika sanaa, nasi tumeona ni
vyema kushirikiana nao ili kuunganisha nguvu, ili kuwaandaa vijana wa
Kitanzania kuwa na ujuzi bora wa sanaa na unaotambulika rasmi,” amesema.
Alisema, uamuzi wa VETA
kuandaa mitaala ya sekta ya sanaa na kuanza kutoa mafunzo kwenye sekta hiyo
umetokana na taarifa za utafiti wa soko
la ajira kubaini kuwa vijana wengi katika sekta hiyo wamekuwa wakifanya
shughuli zao kwa kutumia vipaji walivyonavyo, ubunifu pamoja na ujuzi
walioupata katika mfumo usio rasmi.
“Sasa katika kuweka suala hili vizuri tumeona ujuzi huu uweze kutambulika rasmi kwa kuandaa na kuanza kutoa mafunzo yatakayowawezesha vijana kujifunza na kupata vyeti katika eneo hilo,” ameongeza CPA Kasore.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mkuu wa THT, Kemilembe Mutahaba amesema wameingia makubaliano na
VETA waweze kutumia fursa ya mitaala na mafunzo ya VETA ili vijana wanaowaandaa
na kukuza vipaji vyao waweze kupata vyeti na kutambulika, kwani wamekuwa wakiwapa
mafunzo ya sanaa pasipo kuwapatia vyeti.
“Mara nyingi tumekuwa
tukiwapa mafunzo vijana, lakini hatuwapi vyeti vinavyotambulika na Serikali.
Tumewekeza bidii zetu kuwawezesha vijana kuajirika kupitia vipaji vyao, kupitia
ushirikiano huu tutaweza kuwasaidia kupata vyeti na kutambulika rasmi,"
amesema.
Naye Mkurugenzi wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dkt. Abdallah Ngodu alifafanua kuwa mitaala
iliyoandaliwa ilizingatia taarifa za utafiti wa soko la ajira uliofanyika mwaka
wa fedha 2022/2023 na kubaini kuwa vijana wengi nchini wanafanya kazi za sanaa,
hasa muziki bila kupitia kwenye mfumo rasmi wa mafunzo.
Dkt. amesema taarifa za
soko la ajira ziliainisha mahitaji ya ujuzi na baada ya kuchakatwa, wataalamu
wabobevu kwenye sekta ya sanaa walishirikishwa katika kuandaa mitaala.
Ameongeza kuwa rasimu
za mitaalaa zilipelekwa kwenye Kamati ya Ushauri ya Kisekta ili kupitia na
kupata maoni na zinatarajiwa kupelekwa kwenye kikao kijacho Bodi kwa idhini,
kisha Baraza la Taifa ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET)
kwa ajili ya kuridhiwa na kupewa ithibati.
No comments:
Post a Comment