CONTACT US: VETA Head Office, P.O.Box 802 Dodoma Tanzania, Plot No. 18, Central business Park (CBP). E-mail: info@veta.go.tz / pr@veta.go.tz/ Telephone: +255 26 2963661 Mobile +255 755267489 Fax: +255 22 2863408 / Url: www.veta.go.tz

Monday, 19 August 2024

MHE. KIPANGA: VIJANA CHANGAMKIENI FURSA ZA MAFUNZO KATIKA CHUO CHA MAFIA

 

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Juma Kipanga ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mafia amewashauri vijana na wakazi wa wilaya ya Mafia kuchangamkia fursa za mafunzo zinazotolewa na Chuo cha VETA Mafia. 

Mhe. Kipanga ametoa kauli hiyo tarehe 17 Agosti, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa Mafia alipokuwa akifungua programu ya mafunzo Jumuishi kwa Ajili ya Kukuza Ujasiriamali (INTEP) kwa kozi za udereva wa bodaboda, mapokezi na hoteli, Usafi na Utunzaji wa Vyumba, Ufuaji wa Nguo, Urembo na Utunzaji wa nywele ambazo zinatolewa chuoni hapo.

Mhe. Kipanga ameongeza kuwa mahitaji ya mafunzo ya ufundi stadi katika wilaya hiyo ni makubwa na kuishukuru VETA Kanda ya Mashariki kwa uamuzi wao wa kutoa mafunzo hayo katika wilaya ya mafia ambapo utaisadia kuongeza maarifa na ujuzi kwa wakazi wa Wilaya hiyo. 

“Chuo hiki cha VETA Mafia kimejengwa kwa ajili yenu na ubora wake ni wa hali ya juu mtu yoyote anaweza kusoma katika chuo hiki, ‘Charity begins at home’ ndugu zangu uzalendo unaanzia nyumbani nawasihi sana tuwalete watoto wetu hapa wapate maarifa, chuo kinapokea watu rika, jinsia na umri wowote, hakuna ubaguzi,” amesema Mhe. Kipanga.

Mhe. Kipanga ameongeza kuwa awali ilikuwa ni changamoto kwa vijana wa bodaboda kupata leseni kwa kuwa hakukuwa na chuo kinachotoa mafunzo ya udereva lakini uwepo wa chuo cha VETA Mafia utatatua changamoto hiyo.

Mhe. Kipanga amefafanua kuwa Wilaya ya Mafia inapokea wageni wengi wanaokuja kwa shughuli za utalii ambapo wataalamu wenye ujuzi wa masuala ya ukarimu, hoteli na utalii wanahitajika katika kutoa huduma bora hivyo mafunzo yanayotolewa kwenye  chuo hicho yataimarisha namna watalii wanavyopokelewa na kuhudumiwa.

Mhe. Kipanga amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa vyuo vya VETA nchini ambavyo vimekuwa kimbilio la wananchi wengi nchini na kuongeza kuwa mafunzo hayo yanayotolewa na kwamba wananchi watatakiwa kufika tu chuoni hapo. 

Naye, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa VETA Kanda Mashariki, Ndugu Alban Kisomba ,amesema VETA ilizindua mafunzo ya INTEP yenye lengo la kuwapatia ujuzi kundi la sekta isiyo rasmi ili kukuza shughuli zao za ujasiriamali.

Kisomba alitumia fursa hiyo kuwasihi wananchi wa Mafia kuchangamkia fursa mbalimbali zinazoletwa na Serikali yao kwasababu nia ya serikali ni kusambaza elimu ya ufundi kote nchini.

Naye kaimu Mkuu wa chuo hicho, Ndugu Salim Jumbe, alisema mafunzo kupitia kozi hizo tano yataendeshwa chuoni hapo kwa muda wa mwezi mmoja na watakuwa wakishirikiana na wadau mbalimbali kama vile Jeshi la polisi kwa ajili ya kuwanoa madereva na Hoteli ya Shugimbili hotel katika kufundisha maswala ya ukarimu na hoteli.

Chuo cha VETA Mafia kilianza kutoa mafunzo mwaka 2023 na kimejengwa na Serikali kwa gharama ya Tshs bil. 2.8 mpaka kukamilika kwake.



No comments:

Post a Comment