Mamlaka ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeingia ushirikiano na Kampuni ya YUNIVESO kwa
lengo la kushirikiana katika nyanja mbalimbali ili kuwezesha mafunzo na
kuwajengea umahiri wanafunzi na wahitimu wa ufundi stadi nchini.
Hati ya makubaliano
ya ushirikiano huo imesainiwa na pande zote mbili, leo, tarehe 24 Oktoba 2024,
kwenye ofisi za VETA Makao Makuu, Jijini Dodoma.
Hati ya makubaliano inataja lengo kuu la ushiriano kuwa ni kuimarisha utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kupitia uandaaji na utekelezaji wa mitaala, uandaaji maandiko na utekelezaji wa miradi kwa pamoja, kubadilishana utaalamu na uzoefu katika utoaji, ugharamiaji na ukuzaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini.
Akizungumza baada ya
zoezi la utiaji saini, Mtendaji Mkuu wa YUNIVESO, Bi Fatma Mshinda amesema
miongoni mwa mchango wa YUNIVESO katika ushirikiano huo ni kuwawezesha wahitimu
wa VETA kupata uatamizi ili kujijenga kiujasiriamali,na kuwatafutia fursa za
kushiriki matamasha mbalimbali ili waweze kuelezea shughuli zao na kuweza
kumudu ushindani kitaifa na kimataifa.
“Sisi hatuna utaalamu wa kutoa mafunzo, hivyo
kazi ya kutoa mafunzo itabaki kwa VETA na sisi tutawawezesha wahitimu kutoka
VETA kupata ajira na fursa mbalimbali,” Bi Fatma ameongeza
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA. Anthony Kasore amesema Kupitia makubaliano hayo,
itasaidia vijana wa Kitanzania kupata ujuzi utakaowezesha kujiajiri na
kuajiriwa, hivyo kupunguza tatizo la ajira nchini.
YUNIVESO ni kampuni ya Kitanzania inayojishughulisha na utoaji ushauri wa kimkakati, kusaidia uendelezaji shughuli za taasisi na ujasiriamali nchini.
No comments:
Post a Comment