Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, leo, tarehe 3 Oktoba 2024 ametembelea na kukagua Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Njombe kilichopo eneo la Shaurimoyo, wilayani Ludewa.
Akiwa chuoni hapo,
Prof. Mkenda ameipongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa
juhudi zake za kuboresha elimu ya ufundi stadi nchini, huku akiagiza mamlaka
hiyo iangalie kwa makini mahitaji ya ujuzi katika jamii ya Ludewa na Njombe kwa
ujumla, akitolea mfano mradi wa uchimbaji na uchakataji wa chuma uliopangwa
kufanyika katika eneo la Liganga, pamoja na shughuli za kuongeza thamani ya
mazao ya misitu.
Aidha, Prof. Mkenda
amewaomba wananchi wa Njombe kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kutokana na jitihada zake za
kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanapata mafunzo ya ujuzi ili kuwawezesha kuwa
na uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa kwa urahisi.
“Kwa Rais ambaye anafanya kazi nzuri kama hii,
ni muhimu kumuunga mkono. Tusipojifunza kusemea mazuri ambayo yanafanywa,
watakuja watu ambao watasema mabaya na kufanya ionekane kazi haifanyiki,”
ameongeza.
Akizungumzia shughuli
za chuo hicho, Waziri Mkenda ameonesha matumaini kuwa chuo cha VETA Mkoa wa
Njombe kitakuwa kiungo muhimu katika kuwaandaa vijana wa mkoa wa Njombe na
maeneo jirani kwa ajili ya fursa za kiuchumi zinazotarajiwa kutokana na miradi
mikubwa inayokuja.
Kwa upande wake, Mkuu
wa Wilaya ya Ludewa, Olivanus Thomas, ameongeza ushauri wake kuhusu maeneo ya
kipaumbele katika mafunzo ya ufundi yanayopaswa kutolewa chuoni hapo akisema ni
muhimu kuzingatia mafunzo yanayohusiana na ujuzi unaohitajika kwenye miradi ya
madini, hasa kwa kuzingatia uwepo wa miradi mikubwa ya uchimbaji inayotarajiwa
kuanza katika eneo la Liganga.
Aidha, Thomas
ameshauri mafunzo yahusishe pia utengenezaji wa vifaa vya uvuvi na ufugaji wa
samaki, ikiwemo vizimba, kwa kuwa wananchi wengi wa Ludewa na maeneo ya jirani
wanazungukwa na Ziwa Nyasa.
"Ni muhimu
kuhakikisha vijana wanapata mafunzo ambayo yatawawezesha kuzitumia ipasavyo
fursa hizi za asili zilizopo katika maeneo yetu," amesema Mkuu huyo wa
Wilaya.
Naye Mbunge wa
Ludewa, Mheshimiwa Joseph Kamonga, alipokuwa akizungumza mbele ya Waziri,
ameeleza kuwa tayari amekubaliana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Wilaya ya Ludewa kuwa eneo linalozunguka Chuo cha VETA Mkoa wa Njombe lipangwe
rasmi ki-mji na kupimwa, hatua ambayo amesema
imelenga kuleta maendeleo katika mazingira ya chuo hicho kwa kuboresha miundombinu
na fursa za kiuchumi kwa jamii ya inayozunguka chuo.
Mbunge Kamonga pia
ametoa ombi maalum kwa Waziri Mkenda kusaidia ukamilishaji wa kituo cha afya
ambacho ujenzi wake ulianza kwa nguvu za wananchi, ili kuhakikisha upatikanaji
wa huduma za afya kwa wanafunzi, walimu, na jamii inayozunguka chuo hicho.
Katibu Tawala wa Mkoa
wa Njombe, Judica Omary, amezungumzia umuhimu wa kupanua mafunzo ya ufundi wa
umeme katika chuo hicho na maeneo mengine ya mkoa, akibainisha kuwa Njombe ina
wazalishaji wengi wa umeme, jambo ambalo linatoa fursa kubwa kwa vijana
kujifunza kwa vitendo na kuendeleza ujuzi huo.
Omary amesisitiza
kuwa ni muhimu kushirikiana na wazalishaji wa umeme ili kuhakikisha vijana
wanapata mafunzo ya kiufundi yanayowezesha kukidhi mahitaji ya soko na
kuwezesha kurithisha ujuzi wa asili kutoka kwa wazee wa mkoa huo, ambao
wamekuwa na uzoefu wa muda mrefu katika kazi za uzalishaji umeme.
"Hili litasaidia
si tu katika kuendeleza maarifa, bali pia kutunza urithi wa kiufundi kwa vizazi
vijavyo," alisema Judica Omary.
Mradi wa Ujenzi wa
Chuo cha VETA Mkoa wa Njombe unatekelezwa na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi
(FDC) Njombe na umefikia asilimia 95 ambapo baadhi ya miundombinu ya chuo
imeruhusu mafunzo kuanza kutolewa.
Akitoa taarifa kuhusu
kuanza kwa Mafunzo chuoni hapo, Mkuu wa Chuo cha VETA Mkoa wa Njombe, Wilfred
Mwatulo amesema chuo kilianza na Mafunzo ya muda mfupi ambapo vijana 14
wamehitimu katika fani za Matumizi ya Kompyuta; Utengenezaji Kompyuta na Umeme
wa Majumbani.
Amesema, Julai mwaka
huu (2024) walidahili wanafunzi 22 wa ngazi ya tatu katika fani ya Umeme na
kwamba mwaka 2025 wamepanga kudahili wanafunzi 200 wa ngazi ya kwanza katika
fani za Uashi, Ufundi Bomba, Umeme wa Majumbani, TEHAMA na Ushonaji, Ubunifu na
Teknolojia ya nguo.
No comments:
Post a Comment